Hamas yaonya, Msikiti wa al-Aqsa ni mstari mwekundu wa Muqawama
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imeonya kuwa, Msikiti wa al-Aqsa ni "mstari mwekundu," na kuahidi kulinda eneo hilo takatifu dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Israel na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni.
Afisa mwandamizi wa Hamas na Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Harakati ya al-Quds, Haroun Nasser al-Din, katika taarifa amesisitiza kwamba, eneo hilo takatifu linasalia kuwa kipaumbele chao cha kidini na kitaifa.
"Al-Aqsa ni mstari mwekundu. Hatutaruhusu mipango mibovu ya uvamizi dhidi ya Msikiti na dhidi ya Quds kupita, bila kujali gharama zake," Nasser al-Din amesema. Amelaani kile alichokitaja kuwa ni kushadidi juhudi za vikosi vya polisi vya Israel vinavyokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, na walowezi kuwazuia waumini wa Kipalestina kuingia katika ua la Al-Aqsa na kuliyahudisha eneo hilo takatifu.
"Mashambulizi haya ni sehemu ya mpango wa utaratibu wa uvamizi wa al-Aqsa kuwaondoa watu wake na kuweka udhibiti kamili juu yake," ameongeza. Afisa huyo wa Hamas amepongeza uthabiti wa Wapalestina wanaoendelea kuhamasishwa na kuitikia wito wa kuilinda al-Aqsa licha ya vikwazo, kunyanyaswa na kukamatwa na askari wa Israel. Uimara wao, amesema, unatuma ujumbe wa wazi wa dhamira isiyotikisika ya kuutetea Msikiti wa Aqsa.
Nasser al-Din ametoa wito kwa Wapalestina huko Quds, Palestina iliyokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948, kudumisha uwepo wao huko al-Aqsa na kuzidisha juhudi zao za kukabiliana na majaribio ya Israel ya kuufanya mji huo kuwa wa Kiyahudi na kubadilisha nembo zake za kidini na kihistoria.
Licha ya vikwazo vikali vya kijeshi vya Israel, takriban Wapalestina 40,000 waliswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa ulioko katika eneo la Quds linalokaliwa kwa mabavu.