Takht-Ravanchi: Iran inaendelea kurutubisha uranium na inaunga mkono diplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127958-takht_ravanchi_iran_inaendelea_kurutubisha_uranium_na_inaunga_mkono_diplomasia
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika Masuala ya Kisiasa amesema kuwa licha ya kutokuwa na imani na Washington kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, bado milango ya diplomasia iko wazi. Majid Takht-Ravanchi amesisitiza kuwa: Iran itaendelea kurutubisha madini ya uranium.
(last modified 2025-07-05T07:55:31+00:00 )
Jul 05, 2025 07:55 UTC
  • Majid Takht-Ravanchi
    Majid Takht-Ravanchi

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika Masuala ya Kisiasa amesema kuwa licha ya kutokuwa na imani na Washington kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, bado milango ya diplomasia iko wazi. Majid Takht-Ravanchi amesisitiza kuwa: Iran itaendelea kurutubisha madini ya uranium.

Akizungumza na NBC News, Majid Takht-Ravanchi, ametilia mkazo msimamo wa muda mrefu wa Tehran kwamba Iran haina nia ya kusimamisha urutubishaji wa madini ya uranium.

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza masikitiko yake kutokana na mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Iran akisema, "Tutawaamini vipi Wamarekani? Tunataka kujua ni kwa nini walituhadaa na kufanya kitendo hiki kibaya dhidi ya watu wetu."

Hata hivyo amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado iko tayari kwa mazungumzo na kuongeza kuwa: "Tunaunga mkono diplomasia na mazungumzo, lakini serikali ya Marekani inabidi ituaminishe kwamba haitatumia nguvu za kijeshi wakati wa mazungumzo. Hili ni sharti la uongozi wetu kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya duru ijayo ya mazungumzo."

Takht-Ravanchi amesema: "Sera yetu ya kurutubisha madili ya uranium haijabadilika. Iran ina haki kamili ya kurutubisha madini hayo ndani ya ardhi yake. Kitu pekee tunachopaswa kuzingatia ni kutosonga mbele kuelekea kwenye harakati za kijeshi (katika uwanja wa nyuklia)."

Mamia ya raia wa Iran waliuawa shahidi katika hujuma ya kijeshi ya Israel ikisaidiwa na Marekani dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Utawala wa Kizayuni ulilazimika kukubali usitishaji vita uliotangazwa na rais wa Marekani siku 12 baada ya uvamizi huo kutokana na mashambulizi makali ya makombora ya jeshi la Iran dhidi ya maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hususan Tel Aviv na Haifa.