Wanahabari mashuhuri walaani upendeleo wa BBC unaoiunga mkono Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127906-wanahabari_mashuhuri_walaani_upendeleo_wa_bbc_unaoiunga_mkono_israel
Kundi la wafanyakazi wa BBC na mamia ya wanahabari na watu mashuhuri wameandika barua ya wazi kwa wasimamizi wa shirika la BBC, wakikosoa upendeleo wa wazi wa tasisi hiyo katika kuakisi matukio ya vita vya Gaza na kuonya kwamba BBC imekuwa msemaji wa propaganda za utawala wa Israel.
(last modified 2025-07-04T03:22:49+00:00 )
Jul 04, 2025 03:22 UTC
  • Wanahabari mashuhuri walaani upendeleo wa BBC unaoiunga mkono Israel

Kundi la wafanyakazi wa BBC na mamia ya wanahabari na watu mashuhuri wameandika barua ya wazi kwa wasimamizi wa shirika la BBC, wakikosoa upendeleo wa wazi wa tasisi hiyo katika kuakisi matukio ya vita vya Gaza na kuonya kwamba BBC imekuwa msemaji wa propaganda za utawala wa Israel.

Barua hiyo, ambayo sehemu yake moja imechapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza, inasema: "Tunaelezea wasiwasi wetu mkubwa kuhusu kuchunjwa habari na ukosefu wa uwazi katika maamuzi ya wahariri wa BBC katika kuandika matukio ya Israel na Palestina. Kwa maoni yetu, kukataa kutangaza filamu ya matukio ya kwelii (documentary) "Gaza: Wafanyakazi wa Misaada Wanashambuliwa", ni mfano mmoja tu wa mfululizo wa maamuzi yaliyofanywa kwa kuzingatia ajenda yenye mwelekeo maalumu. Uamuzi huo, kwa mara nyingine, umeonyesha kuwa BBC inafanya kazi kwa njia ya upendeleo wakati wa kuripoti habari kuhusu Israel, kinyume na kauli mbiu yake ya kutoegemea upande wowote."

Waandishi wa barua hiyo wamesisitiza kuwa uamuzi wa BBC wa kutorusha hewani filamu hiyo, licha ya maudhui yake kuidhinishwa kwa mujibu wa miongozo ya ndani ya BBC, ulifanywa na wasimamizi wakuu na unatambuliwa kuwa uamuzi wa kisiasa unaoakisi hofu ya shirika hilo ya kukosolewa na utawala wa Israel.

Sehemu nyingine ya barua hiyo inasema: "Hatutarajii BBC kuwa na upendeleo, lakini badala yake ituruhusu kufanya kazi kwa uwazi na kwa usahihi."

Waandishi wa barua hiyo wameeleza kuwa katika kuangazia matukio yanayohusiana na Palestina, BBC imefeli katika kutoa uchambuzi wa maana kuhusu nafasi ya serikali ya Uingereza katika vita hivi, uuzaji wa silaha, au athari zake za kisheria..

Waliotia saini barua hiyo wameonya kuwa mwenendo huo wa BBC haukutokea kwa sadfa bali umefuata mpango mahususi.

Barua hiyo ya wazi ya kupinga upendeleo wa BBC kwa utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina imetiwa saini na wanahabari wasiopungua 112 wa sasa na wa zamani wa BBC, pamoja na zaidi ya waigizaji 300, watengenezaji filamu, maprofesa wa vyuo vikuu, wanaharakati wa vyombo vya habari na waandishi wa habari wa kujitegemea.