Al-Houthi: Naukubali mwenendo wa Iran dhidi ya adui
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi, amezungumzia vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wake dhidi ya Iran na kusisisitiza kuwa "mfano wa Iran" umeonyesha kuwa nguvu ni matokeo ya muongozo wa Mwenyezi Mungu, uamuzi sahihi na ustahamilivu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Watu wa Yemen amesema: "Moja ya vipengee vikuu vya nguvu ya Iran ni kuwa thabiti katika misimamo yake. Badala ya kurudi nyuma au kufanya mapatano na adui, Wairani waliamua kutoa jibu madhubuti, na jibu hilo kali lilimlazimisha adui kusimamisha mashambuulizi yake licha ya misaada na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Magharibi."
Sayyid Abdul Malik amesema: "Israel haikuweza kuendelea na mashambulizi yake kutokana na gharama kubwa ilizolipa kutokana na uchokozi huo. Suala hili linadhihirisha wazi kwa Umma wa Kiislamu umuhimu wa kujiandaa kijeshi na kuwategemea wananchi."
Ametilia mkazo utayarifu kamili wa Iran kwa ajili ya jibu la kuangamiza zaidi iwapo Israel itafanya mashambulizi tena na kuongeza kuwa: Iran iko katika nafasi ambayo inaiwezesha kufanya mashambulizi makali zaidi kuliko hapo awali dhidi ya adui Mzayuni.
Akizungumzia hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, Al-Houthi amesema, adui Mzayuni amekuwa akiendeleza mauaji ya kimbari ya wananchi wa Palestina mbele ya macho ya Waislamu kwa zaidi ya miezi 21.
Amelaani mashambulizi ya utawala huo dhidi ya taasisi, makazi na kambi za wakimbizi, shule na maeneo mengine ya umma akisema hatua hizo ni dhihirisho la wazi la jinai, ukatili na unyama usio na mipaka.