Israel yaua shahidi Wapalestina 64 katika Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i127970
Mashambulizi ya Israel yamesababisha kuuawa shahidi Wapalestina 64 katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza tangu alfajiri ya leo Jumamosi, huku makumi ya waliouawa wakitambuliwa kama waombaji misaada, kwa mujibu wa ripoti kutoka hospitali za eneo hilo lililozingirwa.
(last modified 2025-07-05T15:25:57+00:00 )
Jul 05, 2025 15:25 UTC
  • Israel yaua shahidi Wapalestina 64 katika Ukanda wa Gaza

Mashambulizi ya Israel yamesababisha kuuawa shahidi Wapalestina 64 katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza tangu alfajiri ya leo Jumamosi, huku makumi ya waliouawa wakitambuliwa kama waombaji misaada, kwa mujibu wa ripoti kutoka hospitali za eneo hilo lililozingirwa.

Mashambulizi haya yametokea katika Ukanda wa Gaza kutoka mji wa Gaza kaskazini hadi karibu na Rafah, kusini mwa eneo hilo.

Vyanzo vya matibabu katika hospitali ya Nasser vimeviambia vyombo vya habari kuwa Wapalestina tisa wakiwemo watoto watatu wameuawa shahidi na wanajeshi wa Israel karibu na kituo cha kusambaza msaada kaskazini mwa Rafah.

Chanzo cha matibabu katika hospitali ya al-Ahli kinasema Mpalestina mmoja aliuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la Israel kwenye kitongoji cha Zeitoun katika mji wa Gaza.

Aidha takriban watu sita wameuawa na zaidi ya 10 kujeruhiwa katika shambulizi la makombora la Israel dhidi ya mahema ya wakimbizi wa ndani waliohamishwa katika eneo la al-Mawasi magharibi mwa mji wa Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, kulingana na Kituo cha Matibabu cha Nasser. Ikumbukwe kuwa, Al-Mawasi iliainishwa kama "eneo la kibinadamu" na Israel.

Vikosi vya Israel kadhalika vimeshambulia shule ya al-Shafi na kuua takriban watu watano na kuwajeruhi wengine kadhaa katika kitongoji cha Zeitoun katika mji wa Gaza.

Utawala katili wa Israel unaendeleza umwagaji damu huu kabla ya Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu kuelekea Marekani siku ya Jumatatu kwa mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Donald Trump yanayotazamiwa kujadili mpango wa kusitisha vita huko Gaza ambavyo hadi sasa vimeshapelekea kuuawa shahidi Wapalestina wasiopungua 57,300 na kujeruhiwa wengine 135,625.