Harakati za Ukombozi Afrika: Magharibi inajaribu tena kugawanya na kutawala Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128906-harakati_za_ukombozi_afrika_magharibi_inajaribu_tena_kugawanya_na_kutawala_afrika
Harakati za ukombozi kutoka nchi sita za Afrika zimekutana mjini Johannesburg, Afrika Kusini, kwa lengo la kuimarisha mshikamano dhidi ya kuingiliwa kwa masuala ya bara hili na mataifa ya Magharibi. Washiriki wameonya kuwa nguvu za kigeni zinajaribu kuligawanya tena Bara la Afrika na kulitawala kiuchumi kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni.
(last modified 2025-07-29T08:00:39+00:00 )
Jul 29, 2025 08:00 UTC
  • Harakati za Ukombozi Afrika: Magharibi inajaribu tena kugawanya na kutawala Afrika

Harakati za ukombozi kutoka nchi sita za Afrika zimekutana mjini Johannesburg, Afrika Kusini, kwa lengo la kuimarisha mshikamano dhidi ya kuingiliwa kwa masuala ya bara hili na mataifa ya Magharibi. Washiriki wameonya kuwa nguvu za kigeni zinajaribu kuligawanya tena Bara la Afrika na kulitawala kiuchumi kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni.

Viongozi kadhaa wa nchi za Afrika, ambao vyama vyao vya ukombozi sasa ni vyama tawala, walikutana Kempton Park, Johannesburg, mwishoni mwa wiki. Walitafakari mchango wao katika mapambano ya ukombozi na kuahidi kudumisha umoja katika kulinda mafanikio ya kidemokrasia dhidi ya ukoloni mamboleo.

Wajumbe hao pia walikumbushana wajibu wao katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Afrika, na kuendeleza ajenda za maendeleo zinazoendana na utu na hadhi ya Mwafrika.

Licha ya changamoto za kisiasa za ndani zinazovikumba baadhi ya vyama hivyo, viongozi walitoa kauli kali dhidi ya kuingiliwa na mataifa ya Magharibi masuala ya Afrika, wakizilaumu kwa kueneza migawanyiko na fitna miongoni mwa mataifa ya Kiafrika.

Kwa kauli moja, vyama hivyo, ambavyo vingi vilikuwa vimewakilishwa na marais wao,  viliahidi kutoruhusu wakoloni kurudi kupitia vikwazo vya kiuchumi na mashinikizo mengine ya kigeni.

Akizungumzia vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa na Rais Donald Trump wa Marekani, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alisema kuwa maadui wa ukombozi hawajawahi kukoma na sasa wanajaribu kufuta historia ya harakati hizo kwa njia ya kisasa.

Mnangagwa amesisitiza kuwa harakati za ukombozi zinahitaji nguvu na mshikamano uleule uliowashinda wakoloni wa jadi, ili kushinda ukoloni wa kisasa unaokuja kwa sura ya biashara na diplomasia kandamizi.

Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah wa Namibia na SWAPO, ameeleza kuwa kuna mikakati ya makusudi kutoka kwa waliokuwa wakipinga uhuru, wanaojificha nyuma ya kisingizio cha maendeleo ya kiuchumi, ushirikiano wa kidiplomasia na sera za mashirika ya kimataifa, ili kudhoofisha mafanikio ya harakati hizo.

Kwa upande wake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa harakati za ukombozi hazipaswi kukubali ukoloni kama hatima ya Afrika.

Ameongeza kuwa: “Tunakumbuka pia kuwa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, ukoloni, na chuki vilifanikiwa kwa sababu ya mshikamano wa kimataifa – hasa kupitia Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) na usaidizi wa ndugu zetu wa diasporani pamoja na marafiki waliokuwa mstari wa mbele.”

Ramaphosa aliwakumbusha wajumbe kuwa mapambano hayakuwa ya kisiasa pekee, bali yalikuwa kwa ajili ya ukombozi kamili wa Mwafrika, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu na kijamii.

Chama cha African National Congress (ANC) kilifunga mkutano huo kwa kukabidhi uenyekiti wa harakati hizo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania, ambacho kitaandaa mkutano ujao.