Hizbullah: Muqawama nchini Lebanon kamwe hautasalimu amri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i127964
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amepinga mwito wa serikali ya Beirut wa kuweka chini silaha kundi hilo la Muqawama na kusema kuwa, "sisi si watu wa kusalimu amri."
(last modified 2025-07-05T15:22:40+00:00 )
Jul 05, 2025 15:22 UTC
  • Sheikh Naim Qassem
    Sheikh Naim Qassem

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Naim Qassem amepinga mwito wa serikali ya Beirut wa kuweka chini silaha kundi hilo la Muqawama na kusema kuwa, "sisi si watu wa kusalimu amri."

Sheikh Naim Qassem amesema hayo akijibu pande zinazoitaka Hizbullah iweke chini silaha, na kuzitaka pande hizo zitoe wito kwanza wa kuondolewa kwa vikosi vamizi katika maeneo yote ya Lebanon.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameeleza kuwa, "Ulinzi hauhitaji ruhusa. Wakati njia mbadala ya kweli ya kutetea nchi inapatikana, basi tunaweza kujadili maelezo yote na wale wanaodai wanaweza kutoa utetezi huo. Tuko karibu, sio mbali, kushiriki katika mjadala huo," kiongozi wa Hizbullah amesema, kwa mujibu wa tovuti ya runinga ya Al-Manar.

 

Akitoa hotuba kwa mnasaba wa maadhimisho ya Ashura ya Imam Hussein (AS) katika Kiwanja cha Sayyed Al-Shuhada, Sheikh Qassem ameeleza kwamba, Hizbullah katu haiwezo kujisalimisha. Amesisitiza kuwa, "Sisi tuko mbali na unyonge!"

Sheikh Qassem amegusia mahesabu ghalati ya baadhi ya vyama vya Lebanon, akisisitiza kuwa pande hizo zimejificha nyuma ya maadui, ili kuwazidi nguvu wafuasi wa Muqawama ambao hawasalimu amri kwa maadui wala kuruhusu dhulma.

Amebaninisha kuwa, "Mafanikio ni wakati tunakomboa ardhi yetu na nchi yetu - huu ni wito wetu kwenu, na sisi tuko tayari."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kwamba, kundi hilo la Muqawama katu halitaitikia wito wa kukabidhi silaha zake kabla ya "kuhitimishwa uvamizi wa Israel" dhidi ya Lebanon.

Wanajeshi wa Israel wamefanya mashambulizi ya karibu kila siku kusini mwa Lebanon, wakidai kulenga ngome za Hizbullah licha ya makubaliano ya usitishaji vita ya Novemba kati ya Israel na Lebanon.

 

Mamlaka ya Lebanon imeripoti kuwa Israel imefanya ukiukaji karibu 3,000 wa mapigano, na kupelekea kuuawa watu wasiopungua 225 na majeruhi kwa zaidi ya 500, tangu makubaliano hayo yatiwe saini.