Equatorial Guinea yaishtaki Ufaransa kwa mahakama ya UN kwa uporaji
(last modified Sat, 05 Jul 2025 15:23:31 GMT )
Jul 05, 2025 15:23 UTC
  • Equatorial Guinea yaishtaki Ufaransa kwa mahakama ya UN kwa uporaji

Equatorial Guinea imewasilisha kesi dhidi ya Ufaransa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikitaka kusitishwa uuzaji wa jumba la kifahari mjini Paris, ambalo nchi hiyo ya Afrika Magharibi inataka kulitwaa tena, mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ilisema hayo jana Ijumaa.

Hii ni hatua ya punde zaidi katika suala linalohusiana na kuhukumiwa nchini Ufaransa kwa Teodoro Nguema Obiang Mangue, mtoto wa rais wa Equatorial Guinea, kwa utakatishaji fedha na ufujaji wa mamilioni ya dola za fedha za umma.

Teodoro Nguema alihukumiwa na mahakama ya Paris mwaka 2017 kifungo cha miaka mitatu jela, na kutozwa faini ya yuro milioni 30. Mahakama hiyo iliamuru kwamba mali zake nchini Ufaransa, zzenye thamani ya makumi ya mamilioni ya euro, zizuiwe, ambayo ni pamoja na jumba la kifahari huko Avenue Foch mjini Paris. Hukumu hiyo ilithibitishwa na kubarikiwa na mahakama ya rufaa mwaka 2020.

Katika kesi iliyowasilishwa Alkhamisi hii, Equatorial Guinea ilisema kuwa ombi lake limetokana na msingi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi, uliopitishwa Oktoba 31, 2003, kulingana na taarifa ya mahakama hiyo.

Equatorial Guinea imesema ombi lake kwa Ufaransa juu ya faili hilo lililopasa kujibiwa kabla ya Juni 27, 2025, lilipuuzwa.

Guinea ya Ikweta inaitaka Ufaransa kuchukua hatua zote kuhakikisha kuwa jengo hilo haliuzwi, kuhakikisha kuwa nchi hiyo ya Kiafrika inalifikia kwa haraka, pasi na kizuizi chochote, na kujiepusha na hatua yoyote ambayo inaweza kuzidisha au kuongeza mzozo.