EU kuchunguza uwezekano wa kuweka vikwazo dhidi ya Israel
Umoja wa Ulaya unatazamiwa kuchunguza suala la kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa utawala ghasibu wa Israel na walowezi wa Kizayuni na kupiga marufuku uuzaji wa silaha kwa utawala huo kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.
Huku kukiwa na ongezeko la ukosoaji wa watu wa Ulaya kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Umoja wa Ulaya unachunguza machaguo matano ya kukabiliana na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel. Hata hivyo, hitilafu za mitazamo miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinadhoofisha uwezekano wa kutekelezwa mpango huo.
Ripoti zinasema kuwa Umoja wa Ulaya unazingatia machaguo matano yanayowezekana kukabiliana na ukiukaji wa Israel wa "kifungu cha haki za binadamu" katika makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini kati ya pande hizo mbili.
Mapendekezo hayo ambayo mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, atayawasilisha kwa mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya, ni pamoja na kusitishwa kikamilifu au kwa sehemu makubaliano ya ushirikiano, vikwazo dhidi ya maafisa rasmi wakiwemo mawaziri na walowezi, vikwazo vya uhusiano wa kibiashara, vikwazo vya silaha na kusimamishwa Israel kushiriki katika miradi ya kisayansi kama vile Horizon Europe.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Baraza la Umoja wa Ulaya mwezi uliopita wa Mei wa kuangaliwa upya uhusiano na Israel, kutokana na "operesheni za kijeshi huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na kuzuia chakula, mafuta na misaada ya matibabu kuingia Ukanda wa Gaza."