Ethiopia kuitosa sarafu ya dola ya US katika miamala ya biashara?
Wizara ya Fedha ya Ethiopia imesema kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki inafanyia kazi hatua za kuiruhusu kufanya biashara kwa kutumia sarafu tofauti isiyo dola ya Marekani, na kwamba kuna nchi ambazo imefikia makubaliano nazo katika suala hili kwa nyakati tofauti.
Wizara hiyo imesema kuwa uamuzi huo unalenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji wa Ethiopia na nchi mbalimbali, kudumisha uwiano wa kibiashara, na kuzuia athari mbaya za utegemezi wa sarafu moja.
Ethiopia imefikia makubaliano na nchi kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu kuziruhusu kufanya biashara kwa kutumia sarafu zao za taifa, amesema Waziri wa Fedha wa Ethiopia, Eyob Tekaign katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Ethiopia.
Tekaign amesema kuwa, serikali inashughulikia njia za kufanya biashara kwa sarafu tofauti na dola ya Marekani ili kurahisisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kwa njia ambayo inalinda maslahi ya Ethiopia.
Haya yanajiri miezi michache baada ya Nigeria ambayo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi barani Afrika, nayo kutangaza kuanza kuuza mafuta ghafi kwa sarafu ya ndani ikiwa na maana ya kuipiga teke na kuitupilia mbali sarafu ya dola ambayo inatumiwa vibaya na dola la kibeberu la Marekani kuyashinikiza mataifa mengine.
Nchi nyingi duniani zikiwemo wanachama wa BRICS, zinajaribu kuimarisha utawala wao wa kifedha na kujikinga na athari hasi za vikwazo vya Magharibi hasa Marekani kwa kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani na kupitisha mbinu mbadala za malipo.