Nguzo za kanisa zaporomoka Ethiopia na kuua watu 36
Takriban watu 36 waliuawa na zaidi ya 200 kujeruhiwa katika tamasha la kidini katikati mwa Ethiopia, wakati viunzi vya mbao vilipowaangukia ndani ya kanisa lililokuwa likiendelea kujengwa.
Tukio hilo lilitokea mnamo asubuhi ya jana Jumatano katika mji wa Arerti, katika eneo la Amhara, yapata ya kilomita 70 mashariki mwa mji mkuu, Addis Ababa.
Kundi la waumini walikuwa wamelitembelea Kanisa la Menjar Shenkora Arerti Mariam kuadhimisha sikukuu ya kila mwaka ya 'Bikira Maria' wakati jukwaa lilipoanguka, huko Minjar Shenkora Woreda, Kanda ya Shewa Kaskazini ya Mkoa wa Amhara.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Ahmed Gebeyehu aliambia shirika la habari la Fana kwamba, watu 36 wamepoteza maisha katika mkasa huo, lakini anasisitiza kuwa idadi ya waliofariki dunia inaweza kuongezeka kwani baadhi ya waliojeruhiwa wapo katika hali mbaya.
"Kilichosababisha maafa ni jukwaa kuporomoka. Liliwakandamiza watu waliokuwa chini. Baadhi ya waliokuwa pembezoni walikimbia nje, lakini waliokuwa katikati waliangamia," amesema Tadesse Tesfaye, aliyenusurika.
Idadi ya watu waliojeruhiwa bado haijafahamika, lakini ripoti zingine zinaonyesha kuwa wanaweza kuwa 200. Afisa wa eneo hilo Atnafu Abate aliambia Shirika la Utangazaji la Ethiopia (EBC) kwamba baadhi ya watu walisalia chini ya vifusi lakini hakutoa maelezo kuhusu shughuli za uokoaji.
Habari zaidi zinasema kuwa, baadhi ya waliojeruhiwa vibaya zaidi walipelekwa hospitalini katika mji mkuu, Addia Ababa.