Ethiopia yaituhumu Eritrea kuwa inajiandaa kuanzisha vita dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131778-ethiopia_yaituhumu_eritrea_kuwa_inajiandaa_kuanzisha_vita_dhidi_yake
Ethiopia imeituhumu Eritrea kuwa inajiandaa kuanzisha vita dhidi yake. Ethiopia imetoa tuhuma hizi dhidi ya Eritrea ikiwa ni ishara ya karibuni ya kushtadi mvutano katika nchi mbili hizo jirani kuhusu udhibiti wa Bahari Nyekundu.
(last modified 2025-10-09T07:13:21+00:00 )
Oct 09, 2025 07:13 UTC
  • Ethiopia yaituhumu Eritrea kuwa inajiandaa kuanzisha vita dhidi yake

Ethiopia imeituhumu Eritrea kuwa inajiandaa kuanzisha vita dhidi yake. Ethiopia imetoa tuhuma hizi dhidi ya Eritrea ikiwa ni ishara ya karibuni ya kushtadi mvutano katika nchi mbili hizo jirani kuhusu udhibiti wa Bahari Nyekundu.

Gedion Timothewos Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia tarehe Pili mwezi huu wa Oktoba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amapo alidai kuwa Eritrea imekuwa ikishirikiana na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF); kundi la upinzani lenye makazi yake huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia. 

Ethiopia pia imeituhumu Eritrea na kundi hilo la upinzani la TPLF kuyafadhili kifedha, kuyapanga na kuyasimamia makundi yenye silaha katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, ambako jeshi la shirikisho limekuwa likipambana na waasi.

Serikali ya Eritrea kwa upande wake haijatoa maelezo yoyote kuhusu tuhuma za Ethiopia dhidi yake. 

Uhusiano kati ya nchi hizi mbili jirani umekwua ukisusua pakubwa zaidi katika miezi ya hivi karibuni.

Itakumbukwa kuwa, Eritrea ilichukua udhibiti wa ukanda wa pwani wa Bahari Nyekundu ilipopata uhuru kutoka Ethiopia mwaka 1993. 

Vita vya mpakani kati ya nchi mbili hizo kati ya mwaka 1998 na 2000 vilipelekea kuuawa makumi ya maelfu ya watu.

Abiy Ahmeda Waziri Mkuu wa Ethiopia alifanya jitihada ili kupunguza hali ya mvutano na nchi hiyo jirani alipoingia madarakani mwaka 2018 hata hivyo katika miaka ya karibuni Ethiopia imekuwa ikifanya kila linalowezekana ili kuweza kuifikia Bahari Nyekundu hatua ambayo imesababisha kusuasua uhusiano wa nchi hiyo na jirani yake Eritrea.  

Katiak barua hiyo kwa Antonio Guterres, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia amesema kuwa nchi yake inatumai kuzungumza na serikali ya Eritrea kuhusu suala hilo.