Wanajeshi wa Nigeria wamuua kamanda wa kundi la kigaidi la Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136180-wanajeshi_wa_nigeria_wamuua_kamanda_wa_kundi_la_kigaidi_la_boko_haram
Jeshi la Nigeria limetangaza Jumapili kuwa vikosi vyake vimemuua kamanda mmoja wa kundi la kigaidi la Boko Haram pamoja na magaidi wengine 10 waliokuwa naye katika operesheni iliyofanyika kaskazini mashariki mwa nchi.
(last modified 2026-02-02T13:56:20+00:00 )
Feb 02, 2026 13:56 UTC
  • Wanajeshi wa Nigeria wamuua kamanda wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza Jumapili kuwa vikosi vyake vimemuua kamanda mmoja wa kundi la kigaidi la Boko Haram pamoja na magaidi wengine 10 waliokuwa naye katika operesheni iliyofanyika kaskazini mashariki mwa nchi.

Katika taarifa yake, jeshi lilisema operesheni hiyo ilitekelezwa katika Msitu wa Sambisa ulioko katika jimbo la Borno.

Kinara wa magaidi aliyeangamizwa ametambuliwa kama Abu Khalid, aliyekuwa naibu kamanda wa Boko Haram katika Msitu wa Sambisa. Alielezwa kuwa mhusika muhimu ndani ya kundi hilo la kigaidi, aliyekuwa na jukumu la kuratibu operesheni na masuala ya vifaa katika eneo la Sambisa.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa hakuna askari wa Nigeria waliojeruhiwa au kuuawa wakati wa operesheni hiyo, huku ikibainisha kuwa oparesheni za kukabiliana na ugaidi zinaendelea katika maeneo yenye misitu kote kaskazini mashariki mwa nchi.

Boko Haram imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, na makumi ya maelfu ya watu wameuawa katika mashambulizi yake tangu mwaka 2009.

Tangu mwaka 2015, kundi hilo pia limefanya mashambulizi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger, na kuua angalau watu 2,000 katika eneo la Bonde la Ziwa Chad.

Mamelfu kwa mamia ya watu pia wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi na mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.