Iran kuzindua satelaiti mpya na kituo cha anga za mbali
Iran inajiandaa kuzindua mafanikio yake mapya katika sekta ya teknolojia ya anga, ikiwemo kuzindua satelaiti iliyotengenezwa ndani ya nchi, picha za kwanza zilizopigwa na setilaiti yake ya hivi karibuni ya Paya, pamoja na kituo kipya cha anga za mbali, katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Anga za Mbali.
Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA), Hassan Salariyeh, amesema kuwa mipango inaendelea ya kurusha satelaiti zaidi angani na kuzindua miradi mipya ya anga kabla ya kumalizika kwa mwaka wa sasa wa kalenda ya Kiirani, unaotarajiwa kuhitimishwa Machi 20.
Alisema mfano mkuu wa kwanza wa mradi wa mfumo wa satelaiti, uliopewa jina la kamanda mashuhuri wa mapambano dhidi ya ugaidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, utazinduliwa kwa mara ya kwanza katika Siku ya Teknolojia ya Anga ya Kitaifa. Aliongeza kuwa Iran pia inalenga kufanya urushaji wa satelaiti kwa kutumia uwezo wa ndani ya nchi, ikiwemo kupitia kituo cha anga za mbali cha Chabahar.
Mfumo huo umetengenezwa kikamilifu na wataalamu wa Kiirani na kwa sasa uko katika hatua ya kukamilika. Unatarajiwa kutoa huduma za kiwango cha juu kwa taasisi za serikali, sekta binafsi, pamoja na wananchi wa kawaida.
Mkuu huyo wa Shirika la Anga za Mbali la Iran amebainisha kuwa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya urushaji wa setilaiti kutoka kituo cha anga cha Chabahar, na uzinduzi wa kwanza utafanyika mara tu satelaiti na chombo cha kurusha satelaiti vitakapokuwa tayari kikamilifu.
Iran iliingia rasmi katika uwanja wa kimataifa wa anga za mbali mnamo Februari 2009, ilipozindua satelaiti yake ya kwanza iliyotengenezwa ndani ya nchi, Omid (Tumaini), ambayo ilitumwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi ya Safir. Satelaiti hiyo, iliyobuniwa kwa ajili ya utafiti na mawasiliano, iliashiria hatua ya kwanza ya Iran katika usindikaji wa data za satelaiti. Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye uwezo wa kuunda na kurusha satelaiti katika anga za mbali na kisha kupokea na kuchanganua data za satelaiti hizo.