DRC yataka maelezo kutoka Uganda kuhusu kufunguliwa mpaka wa Bunagana
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetaka maelezo kutoka kwa serikali ya Uganda, kuhusiana na kufunguliwa kwa mpaka wa Bunagana, katika eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23.
Kufuatia kikao cha Baraza la Mawaziri, Wizara ya Mambo ya nje, imetakiwa kutafuta majibu kutoka kwa serikali ya Uganda ni kwa nini mpaka huo ulifunguliwa tena wiki hii, bila ya kuwepo kwa maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeeleza kushangazwa na uamuzi huo wa Uganda ambao haukumshirikisha Jirani yake huyo.
Mpaka wa Bunagana ulifunguliwa tena siku ya Alhamisi, na maafisa wa serikali ya Uganda, katika eneo hilo ambalo tangu mwezi Juni mwaka 2022 kwa sababu za kiusalama, lipo chini ya waasi wa M 23.
Ripoti zinasema, mpaka huo ulifunguliwa baada ya maagizo ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba baada ya maelekezo ya Rais Yoweri Museveni ili kufungua tena fursa hasa za kibiashara kati ya nchi hizo jirani.
Tangu kufungwa kwa mpaka wa Bunagana, kulisababisha ukosefu wa ajira kwa wenyeji wa Bunagana kutoka pande zote mbili, na kuanza kusababisha umasikini kati ya raia wa kawaida katika eneo hilo la mpakani.
Hata hivyo hatua ya Uganda ya kufungua mpaka huo pasina kuijulisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imezua maswali mengi hasa kwa kuzingatia kuwa, eneo hilo linadhibitiwa na waasi wa M23 wanaoendesha vita dhidi ya serikali ya Kinshasa.