Iran: EU ikishinikiza turejeshewa vikwazo vya UN, tutajitoa NPT
(last modified Thu, 12 Jun 2025 02:53:25 GMT )
Jun 12, 2025 02:53 UTC
  • Iran: EU ikishinikiza turejeshewa vikwazo vya UN, tutajitoa NPT

Iran imeonya kwamba, huenda ikatumia haki yake ya kisheria ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) ikiwa mataifa ya Ulaya yataendelea na jaribio lisilo na msingi wa kisheria la kuamilisha mchakato wa kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katka Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani ametoa indhari hiyo katika barua aliyoliandikia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatano.

Barua hiyo imekuja kujibu msukumo unaoendelea kutolewa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani (Troika ya Ulaya), unaolenga kuhuisha vikwazo dhidi ya taifa hili.

Kampeni hiyo imezifanya nchi tatu hizo za Ulaya pamoja na Marekani kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ili kushinikiza kurejeshwa vikwazo shadidi vya UN dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mashinikizo hayo yanakuja sambamba na madai ya kukaririwa ya washirika hao wa Magharibi dhidi ya Iran, eti inapania kuunda silaha za nyuklia, tuhuma ambazo hazijathibitishwa na shirika la IAEA katika kipindi chochote kile, licha ya kufanya ukaguzi mkali usio na kifani hapa nchini.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katka Umoja wa Mataifa ameshutumu kampeni hiyo ya Magharibi na kuitaja kama "kitendo kisicho na msingi wa sheria na cha kisiasa, ambacho kitakuwa na matokeo mabaya sana kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa."

Huku hayo yakiarifiwa, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa vikali hatua ya kichokozi ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ya kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA, akionya kuwa uamuzi wowote wa "kutozingatia busara" kutoka kwa wajumbe wa bodi hiyo ya wanachama 35 utajibiwa kwa hatua muafaka kutoka Tehran.