Mearsheimer: Marekani haina budi isipokuwa kukubali matakwa ya Iran
-
John Mearsheimer
Msomi na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya siasa za kimataifa wa Marekani, John Mearsheimer, amesema kuwa Marekani haina chaguo jingine bali kukubali matakwa ya Iran.
Mearsheimer amesema kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa na kimkakati yanaifanya Washington ilazimike kuafiki baadhi ya masharti yanayotolewa na Tehran, akisisitiza kuwa Marekani haiwezi kupuuza hali halisi ya nguvu katika eneo la Asia Magharibi.
Mwananadharia huyo wa Marekani katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Chicago amesema ni vigumu kufahamu namna Marekani inavyoweza kupata hata ushindi mdogo katika mzozo wake na Iran.
Mearsheimer amesema kuwa iwapo Washington inataka kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuzuia kutokea janga la kiuchumi, haina chaguo kubwa isipokuwa kukubali karibu matakwa yote ya Iran.
Profesa huyo wa Chuo Kikuu cha Chicago amekumbusha kuwa, mwanzoni mwa vita dhidi ya Iran, Marekani ilikuwa na malengo makuu manne; kuibadilisha serikali ya Iran, kukomesha uwezo wa Iran wa kurutubisha urani, kuangamiza uwezo wake wa makombora, na kusitisha uungaji mkono wa Iran kwa makundi ya Muqawama.
Amesema Marekani haijafanikiwa kufikia lengo lolote kati ya hayo, na kwa sasa hakuna dalili kwamba inaweza kuyatimiza.
John Mearsheimer amesisitiza kuwa Marekani haina chaguo la kijeshi, na kwamba kuongeza mzozo kutakuwa na madhara makubwa kwa Wamarekani.
Kwa upande mwingine, amesema Iran inaamini kuwa ina chaguo la kijeshi na inaweza kubadilisha mizani ya nguvu katika mzozo huo.
Ameongeza kuwa hali ya sasa inaifanya Marekani ikabiliwe na changamoto kubwa katika kufikia malengo yake katika mzozo huo.