Oman: Tishio hatari zaidi halitokani na Tehran bali Tel Aviv
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139888-oman_tishio_hatari_zaidi_halitokani_na_tehran_bali_tel_aviv
Serikali ya Oman imesema tishio kubwa zaidi kwa usalama na utulivu wa eneo halitokani na Tehran, bali linatoka Tel Aviv.
(last modified 2026-07-15T04:02:41+00:00 )
Jul 15, 2026 03:52 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidi
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidi

Serikali ya Oman imesema tishio kubwa zaidi kwa usalama na utulivu wa eneo halitokani na Tehran, bali linatoka Tel Aviv.

Katika taarifa yake, Oman imeeleza kuwa hatua na sera za Israel ndizo zinazochochea kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati, na kusisitiza kuwa juhudi za kidiplomasia na mazungumzo ndizo njia bora za kutatua migogoro na kudumisha amani katika eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidi, amekosoa kuendelea kwa vita katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Ghuba ya Uajemi halitokani na Tehran, bali linatokana na maamuzi na hatua zinazochukuliwa na Tel Aviv.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr likinukuu Al Jazeera, Al-Busaidi amesema kwa sasa kuna mazungumzo tata yanayoendelea kwa lengo la kuandaa utaratibu wa muda mrefu utakaohakikisha uhuru wa usafiri wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Ameongeza kuwa Oman ina wajibu wa kushirikiana na Iran pamoja na jamii ya kimataifa ili kufanikisha utaratibu utakaohakikisha usalama na uhuru wa meli kupita katika njia hiyo muhimu ya kimataifa.

Waziri huyo amesema tishio hatari zaidi kwa usalama wa Ghuba ya Uajemi halitokani na nchi za eneo hilo, bali linachochewa na maamuzi na harakati zinazofanywa nje ya eneo hilo, hususan kutoka Tel Aviv.

Aidha amesema vita vya sasa vimeleta maafa makubwa, havikupata idhini ya Umoja wa Mataifa na havikufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande mwingine, mtandao wa Al Mayadeen umeripoti kuwa Al-Busaidi, katika makala aliyochapisha kwenye gazeti la Le Monde, alisisitiza kuwa tishio kubwa zaidi halitokani na Tehran bali linatoka Tel Aviv. Amesema ni muhimu kujifunza kutokana na hali ya sasa na kuelekeza juhudi katika kujenga mustakabali bora badala ya kuendelea kushughulikia makosa ya zamani.