Qalibaf: Hakuna sababu ya kuendelea kuzingatia makubaliano na Marekani iwapo Iran hainufaiki
-
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf,
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameonya kwamba ikiwa Jamhuri ya Kiislamu haitanufaika na Mkataba wa Maelewano (MoU) wa Islamabad uliotiwa saini baina yake na na Marekani, basi hakuna sababu yoyote ya kuendelea kuufuata.
Katika taarifa iliyochapishwa Jumatano, ambayo iliainisha mtazamo wa kimkakati unaosawazisha utayari wa kijeshi na ushirikiano wa kidiplomasia ili kulinda maslahi ya kitaifa, Qalibaf amesisitiza kuwa MoU hiyo ina maana tu pale vifungu vyake vinapokuwa na uhalali na kutekelezwa.
Amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran vina uhuru kamili wa kuchukua hatua za kukabiliana na uchokozi wowote wa adui.
Kauli ya Spika huyo imekuja wakati mvutano ukizidi kupamba moto kufuatia ukiukaji wa mara kwa mara wa Marekani wa makubaliano hayo ya muda yenye vipengele 14.
Iran imerekodi angalau ukiukaji 42 mkubwa wa Marekani tangu MoU hiyo iliposainiwa tarehe 17 Juni, ikiwemo kukiuka mipango ya Iran katika Lango la Hormuz, vitisho vinavyoendelea vya mashambulizi ya kijeshi, mashambulizi dhidi ya kusini mwa Iran, kurejesha vikwazo vya mafuta, na uchokozi unaoendelea wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon.
Rais wa Marekani Donald Trump pia ametangaza kuwa utaratibu wa kusitisha mapigano na Iran hauko tena katika utekelezaji.
Qalibaf amesisitiza kuwa Iran inapaswa kuzingatia maslahi ya kitaifa na usalama, na si mitazamo ya mirengo au makundi.
Amesisitiza tena kuwa Marekani haijabadilisha mkakati wake wa ubeberu na haitavumilia kamwe Iran imara.
Spika Qalibaf amefafanua kuwa mazungumzo si sawa na kusalimu amri, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa mapambano (muqawama) na kulinda maslahi ya kitaifa.
Ameonya kuwa kutenganisha nyenzo za kijeshi na kidiplomasia na kuchagua moja tu kama suluhisho pekee itakuwa ni makosa ya kimkakati.
Qalibaf amebainisha kuwa Iran ilifanikiwa kufunga Lango la Hormuz wakati wa vita vya siku 40, tofauti na vita vya siku 12, kwa sababu lango hilo la bahari lilikuwa limegeuka kuwa chanzo cha ukosefu wa usalama na tishio kwa usalama wa taifa.
Qalibaf pia amezungumzia suala la kulipiza kisasi kwa ajili ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyekuwa shahidi na mashahidi wengine wa vita hivyo viwili vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na tawala za Marekani na Israel. Amesema kuwa njia ya ushindi iko katika kufuata mwongozo wa Kiongozi mpya, Ayatullah Seyed Mojtaba Khamenei, na ramani sahihi ya njia inayozingatia mapambano (muqawama), mantiki, na matumizi ya busara ya uwezo wote wa kijeshi na kidiplomasia.
Ameitaka jamii ya Iran kudumisha umoja na uwepo wake uwanjani, akipuuza juhudi za adui za kueneza hofu, kukata tamaa, na mgawanyiko.
Mkataba wa Islamabad ulikusudiwa kuweka msingi wa kufungua tena Lango la Hormuz kwa usafirishaji wa kibiashara, kumaliza mapigano, na kuanza mazungumzo kuelekea makubaliano ya mwisho ya amani.
Hata hivyo, Marekani imekiuka makubaliano hayo kwa utaratibu, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ikitangaza kuwa Washington “imevunja kabisa” sitisho hilo la mapigano.