Bunge la Iran lawasilisha muswada wa kusimamia Lango Bahari la Hormuz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139894-bunge_la_iran_lawasilisha_muswada_wa_kusimamia_lango_bahari_la_hormuz
Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limewasilisha rasmi muswada wa sheria unaolenga kuimarisha usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz, hatua inayokuja wakati wa kuongezeka kwa mvutano na uingiliaji wa Marekani katika njia hiyo muhimu ya kimkakati ya baharini.
(last modified 2026-07-15T04:01:17+00:00 )
Jul 15, 2026 03:59 UTC
  • Ukumbi wa Bunge la Iran
    Ukumbi wa Bunge la Iran

Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limewasilisha rasmi muswada wa sheria unaolenga kuimarisha usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz, hatua inayokuja wakati wa kuongezeka kwa mvutano na uingiliaji wa Marekani katika njia hiyo muhimu ya kimkakati ya baharini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, Ebrahim Azizi, alitangaza hilo kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X siku ya Jumanne, akisema kuwasilishwa muswada huo kumekuja sambamba na tukio la kutunguliwa kwa ndege zisizo na rubani za Marekani katika eneo.

“Usiku uliopita, sambamba na kuangamizwa kwa ndege zisizo na rubani za Marekani, mpango wa kimkakati wa kuhakikisha usalama na maendeleo endelevu ya Mlango Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Uajemi ulitangazwa na kupokelewa rasmi katika kikao cha wazi cha Bunge,” amesema Azizi.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa Iran itaendelea kusimama imara katika kulinda kile ilichokiita "mipaka yake isiyoweza kuvukwa", hususan kuhusu usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya usafirishaji wa mafuta duniani.

“Hii ni hatua ya kwanza; hatua nyingine zinafuata,” amesema Azizi, akidokeza kuwa Tehran inaweza kuchukua hatua zaidi katika siku zijazo ili kuimarisha msimamo wake kuhusu usalama wa bahari katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Iran imeendelea kuweka vikwazo katika usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz tangu siku za mwanzo za vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala haramu wa Israel mnamo Februari 28. Vita hivyo vilisitishwa mwanzoni mwa mwezi Aprili baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano, kufuatia ushujaa wa vikosi vya Iran na mafanikio ya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Mnamo Juni 17, Tehran na Washington zilitia saini Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosimamiwa na Pakistan. Kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha makubaliano hayo, jukumu la kufungua tena na kusimamia usafiri katika Mlango Bahari wa Hormuz limekabidhiwa rasmi kwa Iran.