Iran yakemea shambulio la Marekani karibu na hospitali ya watoto huko Ahvaz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139932-iran_yakemea_shambulio_la_marekani_karibu_na_hospitali_ya_watoto_huko_ahvaz
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekemea shambulio la Marekani karibu na hospitali ya watoto wanaougua saratani katika mji wa Ahvaz, kusini-magharibi mwa nchi, na kulitaja kuwa ni “uhalifu wa kivita wa kijinga na wa woga.” Taarifa zinasema shambulio hilo lililazimisha uokoaji wa dharura wa mamia ya wagonjwa walio katika hali hatarishi na pia limewatia hofu watoto wanaopatiwa matibabu ya saratani.
(last modified 2026-07-16T10:44:24+00:00 )
Jul 16, 2026 10:42 UTC
  • Iran yakemea shambulio la Marekani karibu na hospitali ya watoto huko Ahvaz

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekemea shambulio la Marekani karibu na hospitali ya watoto wanaougua saratani katika mji wa Ahvaz, kusini-magharibi mwa nchi, na kulitaja kuwa ni “uhalifu wa kivita wa kijinga na wa woga.” Taarifa zinasema shambulio hilo lililazimisha uokoaji wa dharura wa mamia ya wagonjwa walio katika hali hatarishi na pia limewatia hofu watoto wanaopatiwa matibabu ya saratani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baqaei, amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi kuwa Hospitali ya Shahid Baqaei, kituo cha matibabu ya saratani ya watoto, kiliondolewa wagonjwa usiku kucha baada ya Marekani kushambulia eneo la karibu.

Amesema shambulio hilo limesababisha dhiki kubwa miongoni mwa wagonjwa hao wadogo na kutatiza huduma za matibabu ya kuokoa maisha.

Alisema: “Shambulio hili la kikatili, linalokumbusha uovu wa utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya afya, limesababisha mateso makali na wasiwasi kwa watoto waliolazwa, na kulazimisha uokoaji wa dharura wa wagonjwa 211 wanaopatiwa tiba ya kemia (chemotherapy).”

Ameongeza kuwa: “Huu ni uhalifu wa kivita wa kijinga dhidi ya viumbe wasio na hatia zaidi , watoto ambao wanapambana kwa ujasiri kwa ajili ya maisha yao.”

Pia amezishutumu serikali zinazokemea uvunjifu wa haki za binadamu kwa kuchagua (kwa unafiki).

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje amebainisha: “Wale ambao kila mara wanahubiri kuhusu haki za binadamu, lakini kwa makusudi hufumbia macho kulengwa kwa hospitali na vituo vya afya, wamepoteza kila chembe ya heshima na uaminifu wa kimaadili.”

Wakazi wa Ahvaz waliripoti kusikia milipuko kadhaa usiku wa Jumatano baada ya mashambulizi ya Marekani kulenga sehemu kadhaa za mji huo wa kusini-magharibi mwa Iran, ikiwemo maeneo ya karibu na hospitali hiyo.

Shirika la Habari la Fars limeripoti kuwa makombora kadhaa yaliangukia karibu na Hospitali ya Shahid Baqaei. Wafanyakazi wa afya, wakisaidiwa na familia za wagonjwa, waliwahamisha wagonjwa waliokuwa wamejaa hofu na kuanza kuwapeleka katika kituo kingine cha afya.

Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Ahvaz kilisema hospitali hiyo imesitisha huduma kwa muda baada ya milipuko katika maeneo ya jirani.

Chuo kikuu hicho kilisema: “Kufuatia mashambulizi ya adui dhidi ya mji na milipuko katika maeneo ya karibu na hospitali, kituo hicho kimesitisha huduma kwa muda ili kuhakikisha usalama wa wagonjwa na wafanyakazi.”

Wizara ya Afya ya Iran imesema wimbi la karibuni la uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran limefanya idadi ya majeruhi kufikia zaidi ya 300 kufikia mchana wa Jumatano, huku watu 35 wakiwa wameuawa.

Shambulio hilo karibu na hospitali hiyo limekuja wakati huu wa kushadidi  mvutano katika Lango Hormuz kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha wiki iliyopita. Ikumbukwe kuwa tarehe 28 Februari, Marekani ilifanya shambulio la kikatili katika shule ya msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab, na kuua watu 168, wengi wao wakiwa watoto.