Wafanyakazi wa kukabiliana na Ebola waandamana DRC wakidai mishahara yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139934-wafanyakazi_wa_kukabiliana_na_ebola_waandamana_drc_wakidai_mishahara_yao
Wafanyakazi wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameanzisha mgomo kushinikiza kulipwa mishahara na marupurupu yao ambayo hawajapokea, hatua iliyosababisha kusimama kwa shughuli za kukabiliana na virusi vya Ebola vinavyoenea kwa kasi.
(last modified 2026-07-16T10:46:37+00:00 )
Jul 16, 2026 10:45 UTC
  • Wafanyakazi wa kukabiliana na Ebola waandamana DRC wakidai mishahara yao

Wafanyakazi wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameanzisha mgomo kushinikiza kulipwa mishahara na marupurupu yao ambayo hawajapokea, hatua iliyosababisha kusimama kwa shughuli za kukabiliana na virusi vya Ebola vinavyoenea kwa kasi.

Mgomo huo ulianza mapema Jumatano katika kituo cha matibabu ya Ebola huko Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri mashariki mwa nchi hiyo na kitovu cha mlipuko wa sasa, ambapo waandamanaji walijenga vizuizi na kuchoma matairi kuzunguka kituo hicho cha afya. Hayo yamedokezwa leo Alhamisi  na Eugene Luyeye, afisa mwandamizi wa serikali katika eneo hilo.

Amesema waandamanaji walilalamika kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa wiki kadhaa bila kupokea mishahara na marupurupu yao, huku wakijitosa katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo kila siku.

Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wafanyakazi walio mstari wa mbele, wakiwemo wafanyakazi wa usafi, maafisa wa ufuatiliaji, wahamasishaji na wengine wanaohusika na jitihada za kupambana na ugonjwa huo hatari wakiwa wamebeba mabango, wakipiga filimbi na kuimba nyimbo za maandamano, wakidai malipo yao.

Mwandamanaji mmoja alisema, “Tunahatarisha maisha yetu kila siku ili kuokoa wananchi, lakini tumeachwa peke yetu. Tunafanya kazi bila kulipwa huku familia zetu zikiteseka. Tunachoomba tu ni haki zetu ziheshimiwe.”

Huo ulikuwa ni mgomo wa pili mfululizo baada ya wafanyakazi wa afya katika mji wa karibu wa Rwampara, mji mwingine ulioathiriwa, kuanzisha mgomo kwa malalamiko kama hayo.

Mgomo huo umekuja takriban wiki mbili baada ya Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Roger Kamba, kuahidi wakati wa ziara yake ya mwisho huko Bunia kwamba mipango inaendelea kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi wa afya wanaojihusisha na mapambano dhidi ya Ebola.

Waandamanaji walidai kupewa vifaa vya kujikinga (PPE) ili kupunguza hatari ya maambukizi, na wametoa makataa ya saa 72 kwa serikali kutekeleza matakwa yao.

Mamlaka za afya nchini Kongo zimekuwa zikipambana na mlipuko wa sasa wa Ebola uliosababishwa na virusi vya Bundibugyo tangu Mei 15.

Taarifa ya hivi punde ya hali ya janga hilo siku ya Jumatano ilionyesha kuwa visa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini humo vimefikia 2,011, vikiwemo vifo 754.

Janga hilo limeathiri majimbo matano, ikiwemo Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Tshopo na Haut-Uele.