Jumatatu, 23 Februari, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Jumatatu 5 Ramadhani 1447 Hijria mwafaka na 23 Februari 2026
Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, baada ya Napoleon Bonaparte, kamanda wa jeshi la Ufaransa kuidhibiti Misri, alianza kufanya mashambulio dhidi ya Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina.
Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri ilifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Lakini sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa.
Katika mashambulio hayo, licha ya kuwa awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania bila kusahau kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa. ****
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita sawa na tarehe 4 Esfand 1323 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchei, faqihi na alimu mkubwa.
Alizaliwa yapata mwaka 1240 Hijiria Shamsia katika kijiji cha Dorchei karibu na mkoa wa Isfahan ndani ya familia ya kisomi na uchaji-Mungu. Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi alijifunza kwa baba yake elimu mbalimbali hadi mzazi wake huyo alipofariki dunia, na baada ya hapo akiwa na kaka yake, alifunga safari hadi mjini Isfahan kwa ajili ya kujifunza masomo ya kidini. Licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kimaisha Ayatullah Dorchei alifanya juhudi kubwa katika kusoma elimu za fiqhi na usulu fiqhi ambapo mwaka 1271 Hijiria Shamsia alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya juu. Aliishi mjini Najaf kwa kipindi cha miaka saba akisoma kwa maulama wakubwa kisha akarejea mjini Isfahan na kujishughulisha na ufundishaji wa elimu za Kiislamu ambapo alikuwa na makumi ya wanafunzi mashuhuri.
Ayatullah Sayyid Muhammad Mahdi Dorchei ameacha turathi kama vile kitabu cha 'Kitabut-Twaharah' 'Kitabus-Swalat' na 'Usulul Fiqh.' ****
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Aliaga dunia Paul Claudel mwandishi, mshairi na mwanasiasa wa Kifaransa. Claudel alizaliwa 1868 na akiwa katika rika la ujana alijiunga na shule ya elimu ya siasa.
Mpaka mwaka 1935 Claudel alikuwa mfanyakazi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa na alisafiri katika mataifa mbalimbali kutekeleza majukumu yake ya kikazi. Hata hivyo kuanzia mwaka huo alichukua muelekeo wa fasihi.
Msomi huyyo alikuwa na harakati katika taaluma mbalimbali za fasihi kama mashairi, visa na uandishi na maigizo. ****
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Februari 1970, mfumo wa utawala nchini Guyana ulibadilishwana kuwa wa jamhuri na siku hii inajulikana nchini humo kuwa Siku ya Jamhuri.
Pwani ya Guyana ilivumbuliwa na wavumbuzi wa Kihispania. Mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, Uingereza iliikoloni nchi hiyo hadi mwaka 1966 ilipojipatia uhuru wake. ****
Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, yaani tarehe 4 Esfand 1358 Hijiria Shamsia, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini MA baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia. ****
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, Abdul-Malik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi linalojiita Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni ya kipekee na ngumu ya kiintelijinsia iliyofanywa na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran na baadaye wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuiteremsha.
Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake kufanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo.
Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti kupambana na ugaidi duniani. *****