Aug 23, 2023 23:01 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 24 Agosti, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Safar 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Agosti 2023.

Katika siku kama ya leo miaka 1395 iliyopita, yaani tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake, Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as).

Baada ya kuuliwa Imam Ali (as), Waislamu walimpa baia na mkono wa utiifu Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza;  hata hivyo baada tu ya kushika hatamu alikabiliwa na njama na uasi wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi kwa ajili ya kukabilina na uasi wa Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.

Imam Hassan al Mujtaba (as) alilazimika kufanya suluhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uislamu na Waislamu. Mjukuu huyo kipenzi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina. 

Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas

Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha. 

Sayyid Ali Andarzgu

Na siku kama leo miaka 32 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake.