Jul 11, 2026 07:51 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumamosi 26 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria sawa na 11 Julai 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa kwa mawe ya moto baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Bani Umayyah, Yazid bin Muawiya. Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika jangwa la Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mawe ya moto.   

***

Katika siku kama ya leo miaka 782 iliyopita, mji wa Baitul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba.  

***

Miaka 469 iliyopita katika siku kama ya leo, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia.   

***

Miaka 425 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.   

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17.

***

Na miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina, waliuawa kwa umati.

Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wanamgambo wa Kiserbia wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade, waliuvamia mji wa Srebrenica licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitangaza eneo hilo kuwa la amani mwaka 1993 na kutumwa askari wa umoja huo katika mji huo. Waislamu wa mji wa Srebrenica walijaribu kuondoka katika mji huo, lakini watendajinai wa Kiserbia waliwauwa wanaume na watoto wao wa kiume na kuwaruhusu wanawake kuondoka katika mji huo. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica.