Jul 11, 2026 02:55 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2026.

Siku kama ya leo miaka 1353 iliyopita, yaani tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Imam Ali bin Hussein, maarufu kwa lakabu ya Sajjad na  Zainul-Abidin, mtoto wa Imam Hussein bin Ali (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (swa).

Imam Zainul Abidin aliuawa shahidi mjini Madina akiwa na umri wa miaka 38. Baada ya mapambano makubwa ya baba yake katika jangwa la Karbala, Iraq Imam Sajjad alikuwa na jukumu zito la kufikisha ujumbe wa mwendelezo wa malengo ya baba yake, Imam Hussein (as).

Imam Sajjad alifanya juhudi kubwa za kufundisha utamaduni wa Kiislamu na kueneza mafundisho bora ya Qur'ani na Suna za Mtume Muhammad (saw), jambo ambalo lilikuwa sababu ya kubakishwa hai Qur'ani na Suna za Mtume.

Imam Zainul-Abidin alikuwa mashuhuri kwa uchamungu mkubwa na alikuwa mwingi wa ibada ya kusujudu, na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya 'Sajjad' ikiwa na maana ya mtu mwenye kusujudu sana.

****

Siku kama ya leo miaka 1152 iliyopita, wavuvi wa Norway walivumbua kisiwa cha Iceland kilichopo kaskazini mwa bara la Ulaya na karibu na ncha ya kaskazini.

Kisiwa hicho kiliingia katika udhibiti wa Norway mwaka 1261 Miladia na karne moja baadaye, Denmark ikazidhibiti nchi mbili zote yaani, Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilifanikiwa kupata uhuru kamili kutoka kwa mkoloni Mdenmark.   ***

Miaka 285 iliyopita katika siku kama hii ya leo ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering.

Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari.

Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.   ***

Tarehe 25 Muharram miaka 195 iliyopita, lilichapishwa gazeti la kwanza la Iran lililojulikana kwa jina la Kaghaze Akhbar.

Gazeti hilo lilichapishwa na Mirza Swaleh Shirazi mjini Tehran, likiwa na kurasa mbili kubwa. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa mwezi na lilizungumzia habari za Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki.***

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Italia ilijiunga rasmi na Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kipindi hicho Waziri Mkuu wa Italia alikuwa Benito Mussolini ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Ufashisti nchini humo. Kuingia Italia katika vita hivyo hakukumsaidia chochote Hitler, licha ya kwamba kulikuwa na taathira kubwa ya ongezeko la uharibifu.

Hadi kipindi cha miaka mitatu, Italia ilikuwa imepata hasara kubwa katika sekta tofauti, huku Benito Mussolini akiuzuliwa madarakani na mfalme wa wakati huo wa Italia mwezi Disemba mwaka 1943, kufuatia kudhibitiwa na waitifaki ardhi ya kusini mwa nchi hiyo.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kwa mujibu wa mkataba wa vita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.  ***

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza.

Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya, Christopher Columbus, na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa hivyo vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.     ***