Jumamosi, 01 Agosti, 2026
Leo ni Jumamosi 17 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria ambayo inasadifiana na Mosi Agosti 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 552 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi kadhaa kwa lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.
***
Miaka 378 iliyopita katika siku kama ya leo, Uhuru wa Uswisi ulitambuliwa rasmi na siku hii ikatangazwa kuwa Siku ya Taifa ya nchi hiyo. Katika Vita vya Miaka Thelathini vilivyoikumba Ulaya kati ya mwaka 1618 na 1648, Uswisi ilidumisha msimamo wake wa kutofungamana na upande wowote. Kutokana na msimamo huo, baada ya kumalizika vita hivyo, uhuru wa Uswisi ulitambuliwa rasmi kupitia Mkataba wa Westphalia. Uswisi ina eneo la kilomita za mraba 41,293 na iko katikati ya bara la Ulaya. Inapakana na Ujerumani, Ufaransa, Italia na Austria.
***
Katika siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.
***
Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, tangazo la vita la Ujerumani dhidi ya Urusi lilipelekea kuanza rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia. Siku tatu kabla ya hapo, Austria ilikuwa imetangaza vita dhidi ya Serbia, ikidai kuwa hatua hiyo ilikuwa ni jibu la kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo mjini Sarajevo. Baada ya Ujerumani kutangaza vita dhidi ya Urusi na baadaye Ufaransa, mzozo huo ulienea kwa haraka na kuhusisha mataifa makubwa ya dunia.
***
Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.
***
Na tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama.
Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.
***