WHO: DRC inakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa Ebola katika historia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140394-who_drc_inakabiliwa_na_mlipuko_mbaya_zaidi_wa_ebola_katika_historia
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa mlipuko wa Ebola unaoendelea kusambaa kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndio mkubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika rekodi zake zote.
(last modified 2026-08-04T03:03:51+00:00 )
Aug 04, 2026 03:02 UTC
  • WHO: DRC inakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa Ebola katika historia
    WHO: DRC inakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa Ebola katika historia

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa mlipuko wa Ebola unaoendelea kusambaa kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndio mkubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika rekodi zake zote.

Katika taarifa mpya, shirika hilo limebainisha kuwa maambukizi yanaendelea kusambaa licha ya kuwepo kwa juhudi za kukabiliana na janga hilo kwa miezi kadhaa sasa. Mlipuko huu wa sasa, ambao ni wa 17 nchini humo ulioatangazwa rasmi 15 Mei, umeripotiwa kupita kiwango cha maambukizi ya janga la Ebola la mwaka 2018-2020 na kuweka rekodi mpya ya kusikitisha.

Kinachotia hofu zaidi ni aina ya virusi vinavyoenea, ambavyo ni virusi vya Bundibugyo, aina ambayo kwa sasa haina tiba wala chanjo yoyote iliyoidhinishwa duniani. Virusi hivi vilibainika mara ya kwanza katika ukanda wa afya wa Mongbwalu mkoani Ituri, lakini ndani ya kipindi kifupi cha miezi miwili, vimesambaa katika mikoa mitano na kuathiri kanda za afya 49. Mikoa iliyoguswa na janga hili ni pamoja na Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele, na Tshopo.

Takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya ya Kongo zinaonyesha kuwa idadi ya kesi zilizothibitishwa imefikia 3,674, huku idadi ya vifo ikipanda na kufikia watu 1,621. Aidha, wagonjwa 760 bado wapo chini ya uangalizi maalum au wamelazwa hospitalini, huku watu 666 wakiripotiwa kupona. Kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huu kimefikia asilimia 44.1, jambo linaloashiria uzito wa hali ilivyo nyanjani.

Mbali na tishio la moja kwa moja la Ebola, hali ya afya ya uzazi mkoani Ituri imedorora vibaya. Taarifa kutoka kwa Noemi Dalmonte, mwakilishi msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini DRC zinaonyesha kuwa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vimeongezeka mara mbili. Kabla ya mlipuko huu, wastani wa vifo vya uzazi ulikuwa 3.1 kwa wiki, lakini idadi hiyo imepaa hadi vifo 5.8 kwa wiki kati ya mwezi Mei na Julai. Vilevile, idadi ya wanawake wanaofia nje ya vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi 17.4 katika kipindi hicho.

Shirika la Afya Duniani limesisitiza kuwa kuna haja ya dharura ya kuongeza nguvu na rasilimali katika mapambano haya. Ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za DRC, mashirika ya kimataifa, na wadau wa afya duniani unahitajika kwa hali na mali ili kudhibiti mlipuko huu hatari wa Ebola na kunusuru maisha ya maelfu ya raia wasio na hatia katika ukanda huo wa Afrika ya Kati.