Jumatano,08 Julai, 2026
-
Leo katika Historia
Leo ni Jumatano 23 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria mwafaka na 8 Julai 2026 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 239 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".
***
Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita aliaga dunia Pierre Paul Broca, msomi wa Kifaransa na mwanzilishi wa elimu ya kraniolojia (elimu ya fuvu la kichwa). Broca alizaliwa Juni 28 mwaka 1824 huko Ufaransa na baada ya kukamilisha masomo ya msingi na sekondari alijiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kusoma taaluma ya tiba na kuhitimi vyema katika fani hiyo. Baada ya kuhitimu masomo Broca alijishughulisha na kazi ya upasuaji akiwa daktai mahiri. Sambamba na kazi yake hiiyo aliendelea na utafiiti na uhakiki. Utafiti wake huo ulimfanya afikie ugunduzi muhimu.
***
Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, Mkataba wa “Saadabad” ulisainiwa mjini Tehran. Saadabad ni jina la mkataba uliosainiwa 8 Julai 1937 kati ya nchi nne: Iran (chini ya Reza Shah Pahlavi), Iraq (Mfalme Ghazi wa Kwanza), Afghanistan (Mohammad Zahir Shah), na Uturuki (Mustafa Kemal Atatürk), kwa msukumo wa Waingereza na kwa lengo la kuizunguka na kupunguza nguvu ya Umoja wa Kisovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, mataifa haya yalikubaliana kuratibu sera zao za nje na kusaidiana katika kukabiliana na tishio la ukomunisti ambalo lingeweza kutishia moja kati ya nchi hizo. Pia yalikubaliana kutokuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo, na kushauriana katika migogoro yote ya kimataifa inayohusiana na maslahi yao, pamoja na kutofanya vitendo vya uvamizi dhidi ya kila mmoja. Hata hivyo, kivitendo, mkataba huu ulikuwa dhaifu na usio na ufanisi. Iran yenyewe ilishirikiana kwa kiasi kikubwa na Ujerumani, ambayo ilikuwa mpinzani wa Umoja wa Kisovieti, na wataalamu wa Kijerumani walifanya kazi katika taasisi nyingi nchini Iran.
***
Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.
***
Tarehe 8 Julai miaka mine iliyopita, waziri mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe aliuawa kwa kupigwa risasi. Shinzo Abe alizaliwa mnamo Septemba 21, 1954 na aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia cha Liberal cha Japan kutoka 2006 hadi 2007 na kwa mara ya pili kutoka 2012 hadi 2020. Abe ndiye mwanasiasa aliyekalia kiti cha waziri mkuu wa Japan kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo. Shinzo Abe alijulikana kimataifa kwa sera za kiuchumi za serikali yake, iliyopewa jina la utani la Abenomics. Abe aliuawa Julai 8, 2022 karibu 11:30 asubuhi wakati alipokuwa akihutubia kampeni za uchaguzi huko Nara. Abe ni waziri mkuu wa sita wa Japani kuuawa.