Aug 24, 2023 22:54 UTC
  • Ijumaa, 25 Agosti, 2023

Leo ni Ijumaa mwezi 08 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe 25 Agosti 2023.

Katika siku kama ya leo miaka 928 iliyopita sawa tarehe 25 Agosti mwaka 1095, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu, kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi.

Miaka 198 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, Uruguay ilipata uhuru. Tangu Uruguay ivumbuliwe na wagunduzi wa Kihispania mwaka 1516, ilitawaliwa na Wareno na Wahispania. Baina ya mwaka 1810 na 1814 kulitokea uasi uliopelekea umwagaji damu mkubwa, ambapo baada ya matukio hayo, nchi hiyo ilipata huru wa kiasi fulani. Hata hivyo mwaka 1820 Brazil iliikalia tena kwa mabavu na miaka mitano baadaye Uruguay ikajikomboa na kujipatia uhuru kamili.

Katika siku kama hii ya leo miaka 156 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza, Michael Faraday. Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba. Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme. *

Michael Faraday

Na siku kama ya leo miaka 82 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, ikiwa ni wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, majeshi ya nchi waitifaki yaliivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wasiwasi ulikuwa umezikumba nchi za Marekani, Ufaransa na Uingereza kufuatia kusonga mbele vikosi vya Ujerumani katika ardhi ya Umoja wa Kisovieti. Kwani nchi hizo zilikuwa zikitambua kwamba, endapo Ujerumani itaushinda Umoja wa Kisovieti maslahi yao katika eneo la Mashariki ya Kati yangekuwa hatarini. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana madola hayo yakapeleka huko Urusi silaha na vifaa vingi vya kijeshi kupitia ardhi ya Iran. Licha ya Iran kutangaza kutounga mkono upande wowote katika vita hivyo, Umoja wa Sovieti ulianza kuishambulia Iran kutoka upande wa magharibi na mashariki, huku majeshi ya Uingereza yakifanya mashambulio kama hayo kwa upande wa kusini.