Jumamosi, 26 Agosti, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe 26 Agosti 2023 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali. ***

Miaka 1024 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Ali Miskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad." ***

Tarehe 9 Safar miaka 850 iliyopita yaani tarehe tisa Safar mwaka 595 Hijria, alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'. ***
Katika siku kama ya leo miaka 677 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga. ***

Miaka 280 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Ufaransa Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa. Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali. Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye. ***
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano. ***

Katika siku kama hii ya leo miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mehdi Araghi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO). Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alifanya mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah. Mehdi Araghi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi. ***
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia. ***
