Jumatano, Agosti 30, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 13 Safar, mwaka 1445 Hijria, sawa na tarehe 30 Agosti mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1142 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1075 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qur'ani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan. Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908 Miladia, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilifanywa na kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO). Rajai alianza kazi ya ualimu sambamba na kushiriki kwake katika harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah na kuendelea katika njia hiyo hadi palipopatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shahidi Rajai alihudumu nyadhifa za Mbunge, Waziri wa Elimu na Malezi, Waziri Mkuu na hatimaye Rais. Wakati wa kipindi cha Urais wake, Rajai alimteua Dakta Muhammad Javad Bahonar kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Kutokana na juhudi, bidii na ikhlasi waliyokuwa nayo katika kulihudumia taifa la Iran ili kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa mfumo wa Kiislamu hawakufurahishwa na utendaji wao huo na ndio maana katika tarehe kama ya leo, wakatega bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu na kuwauwa shahidi. Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema baada ya kufa shahidi Rajai na Bahonar kuwa "thamani za mabwana hawa Rajai na Bahonar ni hizi kuwa, viongozi hao walikuwa bega kwa bega na wananchi."
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.