Jumatatu, 4 Septemba, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 18 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria, sawa na tarehe 4 Septemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika Vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu SAW, Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu SAW kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Hata hivyo Mtume Muhammad (saw) alimzungumzia Uways na kumsifu licha ya kwamba hakuwahi kuonana naye. Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as), alishiriki kikamilifu kwenye Vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya bin Abi Sufiyan na akauawa shahidi katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa. Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.
Miaka 139 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 18 Mfunguo Tano Safar alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi al Hindi. Alizaliwa mwaka 1246 Hijria nchini India na kupata elimu katika taaluma za fiqhi, Hadithi, teolojia na elimu nyingine za Kiislamu. Miir Hamid Hussein alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufunza elimu za kidini na kuandika vitabu. Kitabu muhimu zaidi cha Allamah Miir Hussein Hindi ni A'baqaatul Anwar. Vitabu vingine vya msomi huyo wa Kiislamu ni pamoja na Asfarul Anwar na Sham'ul Majalis.
Tarehe 4 Septemba miaka 115 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright. Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider.
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa.
Na tarehe 13 Shahrivar miaka 45 iliyopita kulifanyika maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah. Maandamano hayo yalianza baada ya Swala ya Eid-ul-Fitr kutoka sehemu nne za Tehran. Waandamanaji waliokuwa wamebeba picha kubwa ya Imam Ruhullah Khomeini (RA), kiongozi wa hayati wa Mapinduzi ya Kiislamu, walipaza sauti na nara za kudai uhuru, kujitawala na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Maandamano hayo makubwa ya mamilioni, ambayo yalikuwa msingi wa maandamano ya kihistoria ya tarehe 17 Shahrivar ya mwaka huo huo, yalimalizika baada ya Sala ya jamaa ya adhuhuri.
