Sep 10, 2023 22:58 UTC
  • Jumatatu, Septemba 11, 2023

Leo ni Jumatatu, mwezi 25 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria, sawa na tarehe 11 Septemba, 2023.

Siku kama ya leo miaka 225 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, kisiwa cha Sri Lanka kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kiingereza. Kisiwa hicho ambacho kijiografia kipo kusini mwa Bara Hindi, kuanzia karne ya 3 Miladia kilikuwa kikihesabiwa kuwa moja ya vituo muhimu vya kiutamaduni vya Mabudha.

Sri Lanka

Miaka 75 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kiutamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu. 

Muhammad Ali Jinnah

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970. 

Jenerali Agustino Pinoche

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa kuswalisha Swala ya Ijumaa. Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin. Ayatullah Madani alipatia elimu kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha kuelekea Najaf Iraq, ambako aliweza kujipatia daraja ya juu ya kielimu ya Ijitihad. Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na askari wa utawala wa mfalme wa Iran kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz.

Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani

Na miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.