Jumanne, Septemba 12, 2023
Leo ni Jumanne tarehe 26 Safar 1445 Hijria sawa na 12 Septemba 2023.
Miaka 126 iliyopita, inayosadifiana na 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mada za nunurishi au radioactive. Baadaye akishirikiana na mmoja wa wasaidizi wa mama yake, mwanafizikia huyo alifanya utafiti na uhakiki katika uga huo na kupata mafanikio makubwa. Irene Joliot-Curie aliaga dunia 1957.
Miaka 103 iliyopita katika siku kama hii ya leo inayosadifiana na tarehe 21 Shahrivar 1299 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanamapambano katika kipindi cha kupigania katiba, na kukandamizwa harakati ya msomi huyo na wafuasi wake katika mji wa Tabriz, ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujipatia elimu kwa maulamaa wakubwa, Sheikh Khiyabani alianza harakati za kupinga dhulma na ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na tawala za silsila ya Qajar hapa nchini. Baada ya kuusambaratisha udikteta wa Muhammad Ali Shah Qajar na kumlazimisha mtawala huyo kukimbia mwaka 1287 Hijria Shamsia, wananchi wa Tabriz walimchagua Sheikh Muhammad Khiyabani kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Taifa la Iran. Hata hivyo katika siku kama ya leo Sheikh Khiyabani alikamatwa na kuuawa shahidi, wakati alipokuwa akipambana na vikosi vya serikali ya kifalme.
Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Selassie. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia kwa shabaha ya kuyadhibiti. Haile Selassie aliwaajiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya marekebisho ya kidara hatua kwa hatua. Alikomesha utumwa, akafanya marekebisho ya masuala ya kifedha na kuanzisha mfumo wa mahakama nchini Ethiopia. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1935 yalisitisha mpango wake huo na alibakia nje ya nchi hadi mwaka 1941 aliporejea nchini kwa msaada wa Waingereza na kutwaa tena madaraka. Aliendeleza marekebisho yake ambayo zaidi yalijikita katika mji mkuu Addis Ababa na mambo yasio ya msingi huku sehemu kubwa ya Waethiopia wakikosa suhula za kimsingi za maisha. Selassie alikuwa tegemeza sana kwa nchi za Magharibi. Tarehe 12 Septemba mwaka 1974 Selassie aliondolewa madarakati katika mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo na mwaka mmoja baadaye utawala wa kifalme ulikomeshwa kabisa nchini Ethiopia.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Septemba 1977, alifariki dunia Steve Biko mwanaharakati wa kupigania haki za wazalendo wa Afrika Kusini, akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Steve Biko alikuwa kiongozi wa wanafunzi aliyefanya jitihada kubwa za kuwawezesha wazalendo waliokuwa wakibaguliwa wa Afrika Kusini na kuratibu harakati zao. Baada ya kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi, Biko alitambuliwa kuwa shahidi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alikuwa mashuhuri kwa kaulimbiu ya "Weusi ni Uzuri" (black is beautiful) ambayo ililenga kuwapa moyo wazalendo wa Afrika Kusini waliokuwa wakibaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao. ***
Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, nchini Uturuki kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Kenan Evren na kupelekea kuondolewa madarakani Waziri Mkuu Suleyman Demirel na kisha kuundwa serikali ya kijeshi. Kuibuka kashfa ya ufisadi wa fedha na kuendelea hali ya kulegalega kisiasa na kijamii nchini Uturuki kulipelekea kutokea mgogoro wa kiuchumi ambapo hatimaye katika siku kama ya leo Jenerali Kenan aliyekuwa mkuu wa majeshi alifanya mapinduzi. Baada ya mapinduzi hayo, Jenerali Kenan akiwa pamoja na Baraza la watu sita walishika hatamu za uongozi wa nchi. Mbali na Waziri Mkuu kuondolewa madarakani kulitolewa amri pia ya kuvunjwa Bunge sambamba na kupigwa marufuku shughuli za vyama vya siasa na nchi ikawa inatawaliwa na serikali ya kijeshi.