Jumatano, tarehe 13 Septemba, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 27 Safar 1445 Hijria sawa na 13 Septemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 1396 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyodumu kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran kwa kushirikiana na jeshi la taifa walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumtia jela kabla ya kuuawa kwake.

Siku kama ya leo miaka 773 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Sallahuddin Ayyubi. Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.
Miaka 243 iliyopita lifti au elevator kwa kimombo ilivumbuliwa. Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani aliyejulikana kwa jina la John Bikbart. Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza huko katika mji wa Chicago. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini katika masafa marefu. Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889 na ile ya otomatiki mwaka 1915.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.
Na Siku kama hii ya leo miaka 30 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.