Sep 14, 2023 23:00 UTC
  • Ijumaa, tarehe 15 Septemba, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Safar 1445 Hijria sawa na Septemba 15, 2023.

Tarehe 29 Safar miaka 1128 iliyopita aliaga dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan ambaye alikuwa mwanahesabati mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu. Muhammad bin Sinan alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, wanajimu na wataalamu wakubwa na gwiji wa nyota wa Kiislamu. Hakuwa na mfano katika elimu ya hisabati katika zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa nchini Misri na alitumia muda wa miaka 40 kufuatilia sayari na nyota. Abu Abdullah bin Sinan alifanikiwa kuainisha wakati halisi wa mwaka wa jua na ameandika vitabu kadhaa kama vile Taadilul Kawakib na Miqdarul Ittisalat.

Abu Abdullah Muhammad bin Jabir bin Sinan

Miaka 202 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania. Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu ya tiba, virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa trakoma au mtoto wa jicho viligunduliwa. Kugunduliwa virusi hivyo kulienda sambamba na njia za kupambana na ugonjwa huo wa mtoto wa jicho, ambapo maelfu ya watu walikuwa wakipofuka katika pembe mbalimbali duniani kutokana na maradhi hayo. Virusi vya trakoma viligunduliwa na matabibu wawili wa Kiingereza. 

Na siku kama hii ya leo miaka 24 iliyopita sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Burujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu."

Dakta Abdulhussein Zarinkub