Sep 15, 2023 22:49 UTC
  • Jumamosi, 16 Septemba 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 30 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe 16 Septemba 2023 Miladia.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1241 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe". ***

Haram ya Imam Ridha (as) katika mji wa Mash'had

 

Miaka 287 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo. ***

Daniel Gabriel Fahrenheit

 

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, Mexico ilijipatia uhuru. Mexico ilipata uhuru baada ya miaka 300 ya kukoloniwa na Uhispania. Siku hii inatambulika kuwa siku ya kitaifa ya nchi hiyo. Nchi ya Mexico yenye kilomita za mraba 1,958,201 iko Amerika ya Kati na inapakana na Marekani na Guatemala. Akthari ya watu wa Mexico ni Wakatoliki. Mji mkuu wa nchi hii ni Mexico City na sarafu yake ni peso. Wengi wa watu wa Mexico ni wana rangi mchanganyiko na wanazungumza Kihispania. ***

Bendera ya Mexico

 

Miaka 92 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano waliivaia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo. ***

Omar Mukhtar

 

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia.  Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Ufumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75. ***

Sir Ronald Ross

 

Tarehe 16 Septemba miaka 84 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo. ***

Warsaw mji mkuu wa Poland

 

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944. ***

Kuanza utawala wa Muhamma Reza Pahlavi

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando yake. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah. ***

Mtetemeko wa ardhi Tabas

 

Na leo tarehe 16 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni. Siku hii haina historia ndefu ikilinganishwa na matukio mengine ya kimataifa. Siku hii iliainishwa mwaka 1994 wakati nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipokubaliana kutenga siku maalumu ya kulindwa tabaka la Ozoni. Tangu wakati huo nchi zote ziliahidi kuanza kuzalisha na kutumia nyenzo na vitu ambavyo havina madhara kwa tabaka hilo. Lengo la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ozoni ni kuhamasisha kulindwa tabaka hilo muhimu sana linalowalinda viumbe hai ardhini wasiathiriwe na mionzi hatari ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet).