Sep 23, 2023 22:47 UTC
  • Jumapili tarehe 24 Septemba 2023

Leo ni Jumapili tarehe 8 Rabiul Awwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Septemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1185 iliyopita aliuawa shahidi Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume wetu Muhamamd (saw) katika mji wa Samarra nchini Iraq. Imam Askari alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina mwaka 232 Hijria na alishika hatamu za kuongoza Umma baada ya kuuawa baba yake mwema Imam Ali al Hadi (as). Kipindi cha uongozi wa Imam Hassan Askari kilijawa na misukosuko mingi kutokana na kuzaliwa ndani yake Imam wa Zama Mahdi (as). Kwani viongozi wa utawala wa kizazi cha Abbas walikuwa wakichunga mno na kumsaka imam huyo aliyeahidiwa kudhihiri katika aheri zamani. Alisifika kwa elimu, ukarimu na ucha-Mungu. Imam aliuawa shahidi na watawala madhalimu wa Bani Abbas kwa kupewa sumu katika siku kama hii leo.

Katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yaliendelea kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano na siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000. 

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18. Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic. 

Bendera ya Guinea Bissau

Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath nchini Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

Imam Khomeini akiwa Iraq