Sep 24, 2023 23:13 UTC
  • Jumatatu, 25 Septemba, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 144 Hijria, mwafaka na tarehe 25 Septemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1185 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan al Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wachamungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Kwa mujibu wa Hadithi tukufu za Mtume Muhammad (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.

William Faulkner

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa huko Baitul Muqaddas.

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kujiendeleza kielimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia.

Edward Said