Jumatano, tarehe 27 Septemba, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na 27 Septemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.
Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Utalii. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.
