Ijumaa, tarehe 29 Septemba, 2023
Leo ni Ujumaa tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na 29 Septemba, 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 1155 iliyopita alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Jorjani alipata masomo ya kidini kwa Qadhi Mkuu wa mji wa Rei ulioko karibu na Tehran ya leo.
Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi, na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo, kaskazini mashariki mwa Iran.

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia, Enrico Fermi katika mji wa Roma.
Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu alivumbua Kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.
Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Zola alindika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal."
Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad.
Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin (MKO). Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege.
Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr.
Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.

Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake José Eduardo dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo.
Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani.