Mar 01, 2024 08:04 UTC
  • Tuujue Uislamu (8)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Katika sehemu ya 8 ya mfululizo huu juma hili, tutaendelea kutoa hoja kwamba, kila kilichoko katika ulimwengu huu kina sababu na sio kila kisichoonekana basi hakipo. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Kwa mtazamo wa mwanadamu, kila jambo lina sababu yake. Kulingana na hili, hakuna jambo linalojitokeza lenyewe na bila sababu ambayo ni chanzo cha kuwepo kwake. Hii ni kanuni na sheria ya jumla. Imamu Sadiq (a.s.) anaitaja sheria hii kuwa ni sheria ya kusababisha na kwamba kila kisababishwa kinahitaji sababu na kisababishi. Anasema: Sunna na mipango ya Mwenyezi Mungu ina msingi ambao ni kufanya kila kitu kipitie katika sababu. Kwa hiyo ameweka sababu kwa kila jambo.

Hii ina maana kwamba, hakuna jambo linaloweza kufanyika bila sababu. Kwa msingi huu, nidhamu na mipangilio yote ya kustaajabisha ambayo inaonekana duniani lazima iwe na sababu, kwa sababu hakuna akili ya kawaida inayoamini kwamba michoro yote hii ya kushangaza katika milango na kuta inaweza kuweko bila ya kuweko msanii na mchoraji mkubwa yaani msababishaji wake. Hapa tunatoa mfano mwepesi: Jaalia uwepo wa jengo kubwa lililojengwa kwa mujibu wa kanuni za kiufundi na kulingana na mahitaji ya taasisi kubwa. Kuwepo kwa jengo hili kunaonyesha kuwa, kuna mtengenezaji na mjenzi, na mjenzi wake alilijienga kwa kuzingatia kanuni sahihi za uhandisi na usanifu majengo.

Ni jambo lisilokubalika kwa mtu yeyote kwamba, kuna kundi lisilo na ujuzi wala utaalamu wowote wa ujenzi ambalo limeamua kupanga matofali na bila ya kubuni ramani na kwa ajili ya kujifurahisha tu na kisha kwa bahati kukatokea jengo kama hili kubwa, zuri na la kisasa la ghorofa kadhaa. Ikiwa atatokea mtuna  kutoa madai kama hayo, basi tunapaswa kutilia shaka usalama na uzima wake wa kiakili.

Sasa ikiwa katika nidhamu ndogo kama hii haiwezekani kutokea kitu bila sababu na malengo wala haiwezekani kukubali kwamba, hakuna mbunifu wake, mtu anawezaje kufikiria mifumo mikubwa na ya kushangaza ya ulimwengu kama ni mambo yaliyokutokea kwa sadfa na vivi hivi tu bila ya kuweko mbunifu, mjenzi na mwenye ujuzi na maarifa? Nidhamu sahihi inayotawala ulimwengu na mpangilio wa viumbe inashuhudia kwamba, muumba wake ni mwenye nguvu, ujuzi, mbunifu na mwenye hekima.

 

Njia iliyo wazi na rahisi ya kumjua Muumba ni kutafakari na kuwa makini katika ulimwengu wa uumbaji. Kwa kufanya uchunguzi katika matukio ya ulimwengu, tunatambua irada yenye hekima ambayo ina tadibiri kwa ulimwengu, inawapa viumbe uhai, na viumbe vyote vinachukua uwepo wao kutoka kwake. Kwa mujibu wa Imamuu Ali (as) ni kuwa, ingawa macho hayawezi kumuona, lakini yeye ni hakika na iliyopo.

Pamoja na hayo, wakati mwingine watu wanakataa uwepo ambao hauko katika hali ya kuonekana na katika wigo wa hisi zao.

Hapa tunapaswa kuuliza swali nalo ni kuwa, ikiwa hatujafanikiwa kupata sababu ya kitu katika uzoefu na utafiti wa kielimu, je, tunapaswa kukana uwepo wa kitu hicho? Au tunapaswa kusema kwamba bado hatujafanikiwa kupata sababu yake? Mtu mwenye hekima na mwenye kufuata hoja za kielimu, katu haoni kwamba, kutoona au kuhisi kuwa ndio msingi wa kukanusha jambo, na wala hakanushi yale ambayo hayapo katika uwanja wa hisi kuu zake tano za kuona, kunusa, kusikia, kuonja na kugusa.

Vinginevyo, kuna kanuni nyingi za kielimu zinazokubalika ambazo hazithibitishwi uwepo wake kwa hisi kuu na hivyo basi zinapaswa kufutwa zinapaswa kuondolewa kwenye uga sayansi. Kwa mfano, ingawa mawimbi ya sumaku na umeme au elektroni ambayo ni chembe ndani ya atomi yenye chaji hasi na nutroni ambayo ni inayopatikana ndani ya atomi zote hazijaonekana kwa macho, lakini wanadamu wametambua uwepo wake na ufanyakazi wake kupitia athari na matokeo, na hakuna mtu anayekataa uwepo wa viwili hivi. Kama ambavyo, kuna viumbe vingi visivyoonekana katika ulimwengu huu ambapo kutokana na maendeleo makubwa ya kielimu katika zama hizi, imethibitika kwamba, kuna viumbe na vitu vingi vilivyoko katika ulimwengu huu ambavyo havionekani.

 

Katika baadhi ya matukio, jicho la mwanadamu haliwezi kuona uhakika halisi wa maada. Kwa mfano, jicho linaweza kuona mwanga wakati tu urefu wake wa mawimbi unapokuwa kati ya wigo fulani. Kwa sababu hii, jicho la mwanadamu haliwezi kuona urujuani yaani aina ya nuru isiyoonekana na binadamu ila na wanyama mbalimbali na miali isiyoonekana (chini ya upinde).

Ingawa nuru hizi zipo ulimwenguni na zina athari na faida zake.  Kwa lugha nyingine na makini zaidi ni sehemu ya mnururisho wa sumaku na umeme wenye lukoka baina ya nanomita 400 hadi 10, ambayo ni lukoka fupi kuliko urujuani inayoonekana lakini ndefu kuliko eksirei.

Kwa hiyo, ikiwa mtu hawezi kuelewa au kuhisi uwepo kwa kitu kupitia zana na vipimo alivyonavyo, hawezi kukana uwepo wake mpaka awe na sababu ya kimantiki ya kutowezekana kwake.

Siku moja, mtu mmoja kutoka Misri, ambaye alikuwa na fikra na mawazo ya kimaada, alikutana na Imam Sadiq (as). Imam alimuuliza baadhi ya maswali mwanzoni mwa mjadala na mdahalo naye: Je, umewahi kwenda chini ya ardhi? Akajibu: Hapana. Imamu akamuuliza Je, unakijua kilicho chini ya ardhi? Alisema: Sijui, lakini nadhani hakuna kitu chini ya ardhi.

Imamu Sadiq (AS) akamuuliza: Je, umekwenda juu ya mbingu? Akasema: Hapana. Imam akasema: Je, unayajua vilivyoko mbinguni? Yule mtu wa Misri akasema: Sijui, lakini sidhani kama kuna kitu huko pia. Imam akahitimisha kutokana na majibu yake kwamba: Hujaenda mashariki wala magharibi, hukusafiri chini ya ardhi wala mbinguni, basi vipi unakanusha vilivyomo humo? Je, kuna mtu mwenye hekima ambaye anakanusha asichokijua? Sasa fahamu kwamba, sisi hatuna shaka kamwe kuhusu Mungu. Je, huoni jua, mwezi, usiku na mchana, ambavyo vinatembea katika njia zao na havitembei ila katika njia yao zenyewe? Ikiwa vina uwezo wa kuondoka na visirudi, kwa nini vinarudi? Wallahi, hivi vyote havina hiari katika harakati zao, na Mwenyezi Mungu ndiye anayeyafanya matukio haya yatiririke katika mzunguko wake na kuyaamrisha, na ukubwa na adhama ni ya kwake.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Jiungeni nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.