Apr 29, 2024 04:33 UTC
  • Tuujue Uislamu (14)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu

 

Tulisema katika maudhui ya tauhidi kwamba ni muhimu kwa mwanadamu kusoma matukio ya ulimwengu na vilivyomo ili kuelewa ujuzi wa kipekee na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Ulimwengu ni darsa bora na zuri zaidi la teolojia na lugha ya kujieleza ya maarifa na mipango ya Kimungu.

Aya nyingi za Quran zinawataka watu kufikiria juu ya mfumo wa uwepo. Katika Aya hizi, Mungu anataja matukio ya asili kuwa ni ishara Zake ili wanadamu waweze kumjua Mungu zaidi kwa kufikiri na kufikiri ndani yake. Wiki hii pia, tutazungumza juu ya ulimwengu wa ajabu wa wanyama katika muendelezo wa kufahamu madhihirisho ya ajabu ya hekima na nguvu za Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 14 ya mfululizo huu.

 

Katika Qur’ani Tukufu Mwenyezi Mungu anaashiria kuumbwa kwa baadhi ya wanyama. Hakika, katika maisha na muundo na mfumo wa uwepo wa wanyama, kuanzia ngamia hadi wadudu wadogo kama vile mchwa na nyuki, kuna siri na maajabu ambayo yanafikirisha.

Ulimwengu wa uumbaji ni mkubwa sana kiasi kwamba, huenda isiwezekane kuhesabu kwa usahihi idadi ya viumbe hai ndani yake. Wanyama wengine wana uzuri wa kushangaza.

Baadhi pia hujulikana kutokana na manufaa yao kwa wanadamu. Bila shaka umesoma na una maarifa japo kwa mukhtasari kuhusiana na maisha ya wanyama wenye miguu minne wa kufugwa, wanyama wasio na madhara ambao ni chanzo cha manufaa mengi kwetu.

Mungu amewaumba wanyama hawa kwa namna ya kuwafuga na kuwatii wanadamu na ni vigumu kwao kuishi bila wao.

Moja ya faida za wanyama wenye miguu minne kama ng'ombe, mbuzi na kondoo ni kwamba, hutayarishwa kutoka kwao maziwa kikiwa kama kinywaji kitamu na cha kuburudisha.

Maziwa ni chanzo cha chakula cha thamani sana na yana kila aina ya virutubisho na vitu vinavyohitajika kwa mwili wa binadamu.

Kwa hakika Mifugo kama vile ng'ombe na mbuzi hutupatia maziwa ambayo hutusaidia kupata protini ambayo husaidia mwili kukua na pia huulinda mwili dhidi ya magonjwa.

Mbali na kutuipatia nyama, ngozi zao zinaweza kutumika kutengenezea vitu mbalimbali. Aidha bidhaa mbalimbali za chakula hutengenezwa kutokana na maziwa.

 

Tangu kale, wanyama wa miguu minne wa kufuga walikuwa wakitumika kama wenzo na suhula ifaayo ya kusafirisha bidhaa na mahitaji ya kibinadamu. Leo hii licha ya kuweko na vifaa vya hali ya juu katika sekta ya usafirishaji, lakini wanavijiji na wapanda milima hutumia wanyama wa miguu minne kama vile farasi na nyumbu kupita barabara ngumu, haswa katika maeneo ya milimani.

Mwenyezi Mungu anasema katika Surat al-Nahl Aya ya 5 hadi 8 kwamba:

Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala. Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi. Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu. Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na ataumba msivyo vijua.

Hapana shaka kuwa, kwa kuutafakari ulimwengu wa wanyama na jinsi wanavyoishi ikiwa ni pamoja na maarifa waliyonayo ya hata kumtambua adui wao, tunaweza kufikia natija hii kwamba, haya yote hayawezekani kutimia na kukamilika pasi na ya kuweko Muumba na msimamizi wake.

Katika uumbaji wa ngamia, kuna nukta na mambo ya kushangaza. Inapaswa kuona jinsi mwili wa mnyama huyu anayefanya kazi kwa bidii namna ulivyoumbwa. Bila shaka mnatambua kwamba, katika majangwa kuna mimea inayochoma na yenye miiba mikali ambayo kwa kawaida hukua jangwani. Hata hivyo, ni rahisi kwa ngamia kula mimea hii, kwa sababu ndani ya mdomo wa ngamia kuna ngozi ngumu ambayo inaweza kula kwa urahisi mimea mikavu na migumu ya jangwani bila kuharibu, kuumiza au kujeruhi kinywa chake.

 

Kwa hakika ngamia anavumilia joto kali lakini pia baridi. Anaweza kubadilisha halijoto ya mwili wake kati ya sentigredi 34 na 42 kulingana na mazingira.

Umbile la ngamiia linalingana na mazingira ya jangwani. Miguu ya ngamia ni mipana na hivyo kuzuia wasizame chini kwenye mchanga.  Shingo ni ndefu kwa sababu kwa chakula anapendelea majani ya miti na vichaka.

Wakati wa dhoruba ya jangwani, ngamia hufunga pua zake ili kujilinda kutokana na uharibifu wa mchanga na vumbi linalotiririka. Uwezo wa tumbo la ngamia ni mkubwa na ana seli nyekundu za damu za mviringo zinazomuwezesha kunywa kiasi kikubwa cha maji kwa muda mfupi kuliko yale anayohitaji ili kukata kiu yake na kuhifadhi maji mengine katika mwili wake.  Kwa maelezo haya kuhusu sifa za ngamia, ni wazi kwamba muundo wa kimwili wa mnyama huyu umeundwa kwa malengo na kuzingatia hali ya hewa ya jangwani, kwa namna ambayo inastahimili joto kali la jangwa, kiu na matukio makali ya kimaumbile kama vile kimbunga na kkadhalika. Bila shaka, mipango na sayansi ya kipekee ilitumiwa katika uumbaji wa mnyama huyu.

Ni nani hasa aliyemuumba mnyama huyu akiwa na sifa hizi na akatabiri na kuandaa kila kinachohitajika ili kuishi katika mazingira ya jangwani? Katika suala hili, ili kuonyesha uwezo wake wa uumbaji, Mwenyezi Mungu anaashiria uumbaji wa ngamia miongoni mwa matukio mengine na kusema katika Aya ya 17 ya Surat al-Ghashia kwamba:

Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa?

Mifano kama hii inapatikana kwa wingi katika ulimwengu wa ajabu wa wanyama na bila shaka, yote haya ni ishara na dalili za kuweko Muumba wa Ulimwengu huu na pamoja na vilivyomo.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki kwa leo umefikia tamati, hivyo sina budi kukomea hapa. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh