Oct 30, 2024 02:26 UTC
  • Jumatano tarehe 30 Oktoba 2024

Leo ni Jumatano tarehe 26 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na 30 Oktoba 2024.

Siku kama ya leo miaka 981 iliyopita, alizaliwa huko Marv, moja ya miji ya Khurasan ya zamani ulioko Turkmenistan ya sasa, Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi, mtaalamu wa hesabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu.

Qatwan Marvazi alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hesabati, falsafa, fasihi na elimu ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo binafsi alipendelea sana elimu ya tiba. M

arvazi ambaye alikuwa akijishughulisha na kutoa huduma ya tiba katika mji wa Marv aliandika vitabu kadhaa na moja ya vitabu hivyo ni 'Kaihaan Shenakht' ambacho kinahusu elimu ya hesabati. Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi alifariki dunia mwaka 548 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 928 iliyopita alifariki dunia Hassan al-Sabbah mwasisi wa utawala wa Ismailiyah nchini Iran.

Sabbah alizaliwa mwaka 445 Hijiria mjini Qum na akiwa mtoto pamoja na familia yake alielekea mjini Ray, kusini mwa mji wa Tehran. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya dini ya Kiislamu na Ushia. Hata hivyo akiwa kijana alijiunga na madhehebu ya Ismailiyah. Wafuasi wa kundi hilo kinyume na Mashia wengine baada ya Imam Swadiq (as) walikataa kumtambua mtoto wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) yaani al-Imam al-Kadhim (as) kuwa Imam na badala yake wakamtambua mtoto mwingine wa Imam Swadiq, yaani Ismail kuwa ndiye Imam.

Baada ya Hassan al-Sabbah kujiunga na kundi hilo alielekea nchini Misri kwa lengo la kujifunza mafundisho zaidi ya Ismailiyah. Wakati huo viongozi wa Ismailiyah walikuwa ni makhalifa wa utawala wa Fatwimiyah nchini Misri. Mwaka 473 Hassan al-Sabbah alirejea Iran na kuanza kueneza mafundisho ya kundi hilo katika maeneo tofauti ya Iran. Mwaka 483 alidhibiti ngome imara ya Alamūt karibu na mji wa Qazvin na ukawa mwanzo wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Seljuk uliokuwa unatawala Iran.

Utawala wa Ismailiya chini ya uongozi wa Hassan al-Sabbah ulidhibiti pia ngome tofauti za kaskazini mashariki, kusini na hata katikati ya Iran sambamba na kuua viongozi wengi wa utawala wa Seljuk.

Hassan al-Sabbah

Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henry Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.

Dunant alizaliwa Geneva, Uswisi na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita.

Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.   

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, yaani tarehe 9 Aban 1304 Hijria Shamsia, Bunge la Ushauri la Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kumuuzulu Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajar na kutangaza kuufuta kikamilifu utawala wa kizazi hicho nchini Iran kilichobaki madarakani kwa kipindi cha miaka 135.

Baada ya kuondoshwa utawala wa silsila ya Qajar, Uingereza ilifanya njama za kuingilia kati na kuuweka madarakani utawala wa muda nchini ulioongozwa na Reza Khan. Reza Khan alijitangaza kuwa mfalme na kuanzisha silsila ya utawala wa Kipahlavi. Utawala huo wa Kipahlavi uliandaa mazingira ya kuporwa zaidi utajiri wa taifa na kukandamizwa wananchi wa Iran kulikofanywa na madola ya Uingereza na Marekani.

Reza Khan

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 540 baada ya utawala wa Baathi wa Iraq kushambulia meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi.

Azimio hilo lilitolewa kufuatia mashambulizi ya utawala wa Iraq dhidi ya meli za kibiashara katika kipindi cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hujuma ambazo zilikuwa na lengo la kuchafua usalama wa eneo hilo. Azimio hilo lilisisitiza haki ya meli zote za kibiashara kufanya safari kwa uhuru katika maji ya kimataifa na lilizitaka nchi zote kuheshimu suala hilo.

Azimio nambari 540 la Baraza la Usalama pia lilizitaka pande mbili hasimu kukomesha mapigano katika Ghuba ya Uajemi na kuheshimu ardhi ya nchi za eneo hilo. Inafaa kuashiria kuwa, azimio hilo lilitolewa huku utawala wa Saddam Hussein ukizidisha mashambulizi yake dhidi ya meli za mafuta za Iran.

Baraza la Usalama