Jumapili, 28 Disemba, 2025
-
Leo katika historia
Leo ni Jumapili mwezi 7 Rajab 1447 Hijria mwafaka na 28 Disemba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1142 iliyopita alizaliwa Ibn Tarrar mpokezi wa hadithi na mwandishi wa fasihi wa Kiislamu huko Iraq. Bin Tarrar ambaye ni jina lake ni Abul Fat'h Muafi bin Zakaria bin Yahya alikuwa miongoni mwa maulama wa Kishafii na alitabahari katika elimu za fiqhi, hadithi na fasihi. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu vingi katika uwanja wa fiqhi. Vilevile aliandika vitabu katika taaluma ya fasihi ya lugha ya Kiarabu kikiwemo kile alichokiita "al Jalisu Wal Aniis".Bin tarrar alifariki dunia mwaka 390 Hijria mjini Baghdad akiwa na umri wa miaka 85.
Katikak siku kama ya leo miaka 251 iliyopita, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.
Katika siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa Paris kati ya Iran na Uingereza wakati wa utawala wa Nassir al-Din Shah. Eneo la Herat lilikuwa likimilikiwa na Iran kwa muda mrefu, lakini wakati wa utawala wa Muhammad Shah Qajar liliondolewa katika milki ya Iran. Nassir al-Din Shah alikusanya jeshi kuelekea Herat ili kulirejesha chini ya mamlaka yake na akateka mji huo mwezi Safar 1273 Hijria. Hatua hii iliibua radiamali ya kutoka Uingereza na washirika wake, ambao waliteka Kisiwa cha Khark, Bushehr na sehemu za Khuzestan. Kufuatia kuzorota huku kwa uhusiano, Iran ilimtuma mjumbe Paris kutatua mzozo huo, ambapo Mkataba wa Paris ulisainiwa. Chini ya mkataba huu, Iran ilizuiwa kuingilia kati nchini Afghanistan na ililazimika kuachana na madai yake ya Herat. Makubaliano haya yalisababisha kuongezeka kwa ushawishi na upenyaji wa wa Uingereza nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895 kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 alpoondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozi na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya figo.