Spika wa Iran: Israel, US zimekanyaga mstari wetu mwekundu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137104-spika_wa_iran_israel_us_zimekanyaga_mstari_wetu_mwekundu
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Rais wa Marekani, Donald Trump na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu wamevuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu, na watalipa gharama kubwa kwa jinai hiyo.
(last modified 2026-03-01T06:37:04+00:00 )
Mar 01, 2026 06:37 UTC
  • Spika wa Iran: Israel, US zimekanyaga mstari wetu mwekundu

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesema Rais wa Marekani, Donald Trump na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu wamevuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu, na watalipa gharama kubwa kwa jinai hiyo.

"Tumejiandaa kwa senario zote, na hata mipango imefanyika kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei," Ghalibaf amesema katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni ya taifa mapema leo asubuhi.

Ghalibaf ametoa ujumbe huo baada ya kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Katika ujumbe wake, Ghalibaf amesisitiza mwendelezo wa uongozi, umoja wa kitaifa, na azma ya kudumisha njia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema taifa la Iran limeachwa na pengo lisilozibika kwa kuondokewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. 

Ghalibaf ameashiria mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa Israel na Marekani dhidi ya taifa hili na kueleza kuwa, operesheni za Iran zinazolenga milki na maeneo ya Marekani na Israel katika eneo zimeonyesha uwezo wa uendeshaji na mshikamano, na kuwashangaza wachambuzi wa masuala ya kijeshi.

Wakati huo huo, Msemaji wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbia ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vituo 14 vya Marekani vimelengwa katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran Jumamosi.

Katika taarifa yake Jumamosi jioni, msemaji wa Khatam al-Anbia ya SEPAH amesema kwamba mamia ya wanajeshi wa Marekani wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran.

Amesema kwamba, utawala wa kihalifu wa Marekani na utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine tena umethibitisha kwamba wanaelewa lugha ya nguvu pekee.