Jumatatu, tarehe 11 Novemba, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 9 Jamadil Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 11 Novemba mwaka 2024.
Tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa Hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza."
Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi.
Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.
Katika siku kama ya leo miaka 466 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadruddin Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadrul Muta'allihīn au Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu.
Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha.
Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu.
Al Mabdau Wal-Maad, Zadul Musafir na Mutashaabihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadrul-Muta'allihīn.
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitolewa fatuwa ya Marajii Taqlidi wa Kishia na Maulamaa wakubwa wa Iraq kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Uingereza.
Hiyo ilikuwa ni katika kipindi cha kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika zama hizo ardhi ya Iraq ya leo ilikuwa sehemu ya utawala wa Othmania ambapo wanajeshi wake hawakuwa na uwezo wa kulinda ardhi hiyo mbele ya Waingereza.
Licha ya kuwa, Mashia wa Iraq walikuwa wamedhurika kutokana na ubaguzi na udhalimu wa utawala wa Othmania, lakini kutokana na fatuwa ya Maulamaa wao walijitokeza na kukabiliana na uvamizi wa Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo.
Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa.
Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.
Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio, viligunduliwa.
Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno.
Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa.
Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo.
Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.