Dec 26, 2025 02:58 UTC
  • Ijumaa, tarehe 26 Disemba, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe 26 Disemba 2025.

Tarehe 5 Rajab miaka 1203 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu.

Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo.

Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik." 

Miaka 977 iliyopita tarehe 5 Rajab 470 Hijria aliaga dunia Ibn Banna, msomi wa sayansi ya Quran.

 Abu Ali Abdullah ibn Banna, alikuwa msomi wa sayansi ya Qur'ani, Hadithi, faqihi, mtafiti wa historia, maadili, theolojia, na lugha ya Kiarabu, na ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo. Idadi ya vitabu vya Ibn Banna inakadiriwa kuwa juzuu 150, ingawa ni vitabu vitatu tu vilivyohifadhiwa katika mfumo wa hati katika Maktaba Kuu ya Damascus. Ibn Banna alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85.

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Atibbaa mmoja wa matabibu mahiri wa Iran alifariki dunia.

Alizaliwa katika mji wa Tabriz nchini Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali ya kidini alisafiri na kuelekea Najaf, Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Sayyid Ali Mar’ashi alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo huko Najaf na kurejea katika mji alikozaliwa akiwa na shahada ya Ijtihadi. Kutokana na mapenzi yake makubwa kwa elimu ya tiba alielekea Isfahan na kusoma taaluma hiyo kwa muda wa miaka 15.

Alimu huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa ambapo Tarikh Tabriz na Sharh Tib al-Nabbi ni baadhi tu ya vitabu vyake muhimu.   

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan.

Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi.

Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan. 

Tarehe 5 Dei mwaka 1382 Hijria Shamsia, yaani siku kama hii la leo miaka 22 iliyopita, mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 6.8 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika mji wa Bam kusini mwa Iran na maeneo ya kandokando yake.

Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu sehemu kubwa ya mji huo na kusababisha vifo vya watu elfu 41. Makumi ya maelfu ya watu wengine pia walijeruhiwa.

Maafa ya mtetetemo huo wa ardhi yalikuwa makubwa mno kwa kadiri kwamba baadhi ya jumuiya na taasisi za kimataifa zilijiunga na wananchi na serikali ya Iran katika kutoa misaada ya dharura kwa waathiriwa. Mbali na hasara za nafsi na vifo vya maelfu ya watu, mtetemeko wa ardhi wa Bam ulisababisha pia hasara kubwa za kiuchumi na kuharibu jengo la kale la Arge Bam. 

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami.

Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa.

Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo.

Mawimbi ya Tsunami yaliyosababishwa na mtetemeko huo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola.