Nov 26, 2024 02:24 UTC
  • Jumanne, 26 Novemba, 2024

Leo ni Jumanne 24 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na tarehe 26 Novemba 2024.

Katika siku kama ya leo miaka miaka 169 iliyopita, Adam Bernard Mickiewicz mshairi na mwandishi mkubwa wa Kipoland aliaga dunia huko Istanbul uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Othmania.

Alizaliwa mwaka 1798. Kama alivyokuwa baba yake, Mickiewicz naye alikuwa mtu aliyekuwa akipigania uhuru. Aliishi katika zama ambazo nchi yake ya Poland ilikuwa imegawanywa na madola ya Prussia, Russia na Austria na alikuwa akifanya jitihada ili nchi yake iungane tena na kuwa kitu kimoja.

Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana mwaka 1823 alibaidishiwa nchini Russia. Baada ya miaka 6, Adam Mickiewicz alikimbilia nchini Ufaransa na kuanza kufundisha fasihi ya lugha.

Adam Mickiewicz

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo.

Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti. 

Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchill na Joseph Stalin, Tehran

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita Joseph Edward Murray, mwanzilishi wa upandikizaji wa figo duniani, alifariki dunia.

Murray alizaliwa Aprili 1, 1919 huko Massachusetts, nchini Marekani. Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1950, hakuna upandikizaji wa viungo uliokuwa umefanyika duniani hadi Dk. Murray na wenzake katika Hospitali ya Peter's huko Boston walipofanikiwa kufanya hivyo kwa mbwa, kwa kutumia mbinu mpya. 

Desemba 1954, walifanya upandikizaji wa kwanza kwa pacha waliofanana, Richard na Ronald Herrick waliokuwa na umri wa miaka 23, wakati Ronald Lee Herrick alipotoa figo yake moja kwa pacha wake aliyekuwa akikaribia kuaga dunia hapo mwaka wa 1954. Lee Herrick alitambuliwa kuwa mtu wa kwanza duniani kuchangia moja ya viungo vyake kwa mtu mwingine.  

oseph Edward Murray